Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Januari 24, 2025 Local time: 17:52

Obama afuturisha na kuzungumzia uvumilivu wa kidini


Rais Barack Obama na wageni katika futari ya pamoja iliyoandaliwa na White House
Rais Barack Obama na wageni katika futari ya pamoja iliyoandaliwa na White House

Rais Barack Obama wa Marekani alizungumza Jumatatu dhidi ya chuki za kidini wakati wa futari iliyoandaliwa na White House kukaribisha mwezi mtukufu wa Ramadhan.

Wafanyakazi kadhaa wa kidiplomasia, wabunge na wamarekani waislam walialikwa kwenye futari hiyo ambapo ni mlo maalumu unaoandaliwa wakati wa mfungo wa Ramadhan.

Rais Obama
Rais Obama

Bwana Obama alisema futari aliyoandaa ni ukumbusho wa “uhuru ambao unatukutanisha sisi pamoja kama wamarekani” ikiwemo “haki isiyovunjwa ya kuabudu imani zetu kwa uhuru”. Aliwatambulisha idadi kadhaa ya vijana wa kimarekani wanaharakati wa ki-Islam kwa wahudhuriaji, akiwemo Samantha Elauf ambaye alifanikiwa kushinda kesi katika mahakama kuu ya Marekani akitetea haki yake ya kuvaa hijab au kitambaa cha kufunika kichwa baada ya kukataliwa ajira kama muuzaji kwenye duka moja la nguo za reja reja.

Rais Obama alilaani matukio kadhaa ya hivi karibuni yaliyosababisha vifo yanayohusiana na dini ikiwemo mashambulizi ya wiki iliyopita kwenye kanisa la kihistoria la wamarekani weusi huko Charleston katika jimbo la South Carolina ambapo watu tisa waliuawa. “Pale thamini zetu zinapotishiwa, tunaunganika pamoja kama taifa moja” alisema bwana Obama. “Kama wamarekani tunasisitiza kwamba hakuna mtu anayetakiwa kulengwa kwa sababu ya namna alivyo, au namna anavyoonekana, nani anayempenda na namna anavyoabudu. Tunasimama pamoja dhidi ya vitendo hivi vya chuki”.

Rais Obama akisalimiana na Samantha Elauf
Rais Obama akisalimiana na Samantha Elauf

Bwana Obama pia alielezea matatizo ya wakimbizi yaliyochochewa na ghasia zinazoendelea kuongezeka huko mashariki ya kati pamoja na matatizo wanayopata waislamu wa Rohingya huko Mynamar.

XS
SM
MD
LG