Waziri Mkuu wa Norway ameongoza ibada ya kuwakumbuka watu 93 ambao hadi sasa wamethibitishwa kupoteza maisha yao Ijumaa baada ya kupigwa risasi na wengine kuuawa katika shambulizi la bomu, mashambulizi yaliyoshtua taifa ambalo kwa kawaida huwa tulivu. Jens Stoltenberg aliwahutubia mamia ya waombolezaji waliokusanyika katika Kanisa moja mjini Oslo leo Jumapili, akisema kuwa mkasa huo ni wa kitaifa ambapo waliouawa walifahamika na wengi, yeye akiwa mmoja wao. Mfalme wa Norway Harald na Malkia Sonja pia walihudhuria ibada hiyo.Nje ya kanisa hilo raia wa Norway walitiririkwa na machozi huku wakiweka shada za maua na kuwasha mishumaa kwa heshima ya waliouawa katika kisiwa cha Utoeya kusini mwa nchi na shambulizi la bomu katikati ya mji wa Oslo. Televisheni ya kitaifa ya Norway NRK ilisema mmoja wa waliopata majeraha ya risasi ameaga dunia na kufanya idadi ya waliouawa katika kisiwa cha Utoeya kuwa 86 huku shambulizi la bomu likiuwa watu 7.Mtu mwenye umri wa miaka 32 raia wa Norway aliyekamatwa na kuzuiliwa na polisi amekiri kuwa alifanya mashambulizi yote mawili na kuwaambia maafisa wa polisi kuwa hakufanya uhalifu wowote. Anders Behring Breivik anatuhumiwa kulipua bomu lililoharibu ofisi ya Waziri Mkuu na majengo mengine ya serikali na baadaye kwenda katika kisiwa cha Utoeya na kuwapiga risasi vijana waliokuwa kwenye kambi wakishiriki katika program iliyodhaminiwa na chama tawala cha Leba.Breivik anasema alifanya mashambulizi hayo akiwa peke yake lakini polisi wanapeleleza ikiwa wengine walihusika. Anatazamiwa kujieleza mbele ya mahakama Jumatatu ambapo anakabiliwa na mashitaka ya ugaidi.
Waziri Mkuu wa Norway aongoza ibada kuwakumbuka waliouawa Ijumaa