Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 15, 2025 Local time: 12:43

Nkurunziza Ahutubia Taifa na Uchaguzi Kufanyika


Rais wa Burundi, Pierre Mkurunziza, ameshukuru vikosi vya jeshi vinavyo mtii kwa kuzuia jaribio la kumpindua, huku akitoa onyo la kumalizwa kwa maandamano yanayompinga.

Bwana Nkurunziza pia amehusisha maandamano hayo na wale walioshiriki jaribio la mapinduzi.

Kwa mujibu wa mwandishi wetu wa Bujumbura, Burundi, Haidallah Hakizimana, aliyekuwepo ikulu wakati ikitolewa hotuba hiyo, amesema rais Nkurunziza pia amewaomba wananchi kuchangia uchaguzi kutokana na kutokuwepo fedha za kutosha kuendesha uchaguzi huo.

Katika hatua nyingine, marais wanne wa zamani wa Burundi, wamepinga hatua ya Rais Pierre Nkurunziza, kugombania awamu ya tatu kwa kuiita ni kinyume cha katiba.

​Maraisi hao wameonya hatua hiyo kwamba inaweza kuvuruga amani iliyopatikana baada ya kumalizika vita ya wenyewe kwa wenyewe mwaka 2006.

Marais hao wanne waliotia saini barua yao ya kumpinga Nkurunziza, ni Jean-Baptiste Bagaza, Sylvestre Ntibantunganya, Pierre Buyoya, na Dominitien Ndayizeye.

Marais hao walitawala Burundi, katika kipindi cha miaka ya 1976 na 2005, wakati Nkurunziza, alipoingia rasmi madarakani kwa kura ya Bunge.

Bwana Nkurunziza, alirejea katika mji mkuu wa Burundi, Bujumbura leo baada ya jaribio la kumwondoa madarakani kushindikana.

Wakati huohuo shirika la kuhudumia wakimbizi la Umoja wa Mataifa ( UNHCR) limesema kwamba raia wa Burundi wanazidi kukimbia nchini humo toka ilipotokea jaribio la kumpindua rais Nkurunziza.

UNHCR inasema idadi ya wakimbizi nchini Tanzania, Rwanda, na Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imeongezeka na kufikia 105,000 toka ghasia zilipozuka katikati ya mwezi April.

Kwa nchini Tanzania, idadi ya wakimbizi inaelezwa kuongezeka maradufu.

Maafisa wa uhamiaji nchini humo wanasema zaidi ya raia wa Burundi 50,000 wamekimbilia nchini humo kupitia bandari ya Kagunga katika ziwa Tanganyika, na karibu watu 10,000 inaripotiwa wanasubiri kuvuka mpaka kuingia Tanzania.

UNHCR inasema raia wa Burundi 26,300 wameshachukuwa hadhi ya Ukimbizi nchini Rwanda, wakati Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo idadi yao ni 9,000.

XS
SM
MD
LG