Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 22:48

Ghasia Nigeria: Buhari aomba utulivu na ushirikiano


Wananchi wa Nigeria wakiwa katika maandamano katika mitaa ya mji mkuu Lagos
Wananchi wa Nigeria wakiwa katika maandamano katika mitaa ya mji mkuu Lagos

Maandamano hayo yamekuwa mtihani mkubwa kwa rais Buhari, ambaye ni afisa wa jeshi mstaafu aliyeingia madarakani kufuatia ushindi wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na ambaye sasa ni Kamanda Mkuu wa jeshi

Rais wa Nigeria ametoa wito kwa raia wa nchi hiyo kuacha maandamano na kushirikiana na serikali katika kusuluhisha matatizo yanayoikumba nchi hiyo, akisisitiza kwamba serikali imesikia matakwa ya waandamanaji na inayashughulikia.

Buhari amehutubia nchi wakati maafisa wa usalama katika mji mkuu wa Lagos wanapata wakati mgumu kutekeleza amri ya watu kusalia nyumbani kwao katika juhudi za kumaliza maandamano ya kupinga polisi kutumia nguvu kuzidi kiasi.

Milio ya risasi imesikika katika mtaa wa Ikoyi, mjini Lagos huku waandamanaji wakichoma vitu barabarani.

Moto umeripotiwa katika gereza la wilaya huku mojawapo ya maduka makubwa likiteketezwa moto.

Machafuko mjini Lagos, ambao ni mji mkubwa zaidi Afrika, yameongezeka tangu jumatano wiki hii.

Makundi ya vijana waliojihami kwa marungu yamekabiliana na maafisa wa polisi katika baadhi ya mitaa ya Lagos, polisi wakiripotiwa kupiga risasi na kuuwa waandamanaji Jumanne usiku katika wilaya ya Lekki.

Mwito wa Buhari

Katika hotuba yake kwa taifa Alhamisi jioni saa za Nigeria, Buhari aliwaomba vijana “kuacha maandamano na kukubali kushirikiana na serikali kutafuta suluhisho.”

Buhari ameomba jumuiya ya kimataifa “kujua ukweli kwa ukamilifu kabla ya kukimbilia kufanya maamuzi.”

Maandamano ya kupinga polisi kutumia nguvu ambayo yameingia wiki ya pili yalikuwa ya amani hadi pale polisi walipowapiga risasi waandamanaji.

Polisi wanasema baadhi ya wahalifu walikuwa wameanza kutumia fursa ya maandamano kufanya uhalifu.

Majimbo kadhaa ya kusini mwa Nigeria yameweka amri ya watu kusalia nyumbani kwao baada ya wiki mbili za maandamano kote nchini ambayo yalikuwa yamegeuka na kuwa makabiliano kati ya polisi na waandamanaji.

Idadi ya vifo

Kundi la kutetea haki za kibinadamu - Amnesty international, limesema kwamba wanajeshi na polisi wameua karibu waandamanaji 12 katika wilaya ya Lekki, wengine mjini Lagos. Jeshi limekanusha kwamba maafisa wake walihusika kisa hicho wakati maafisa walikuwa wanawatawanya watu waliokuwa wamekiuka masharti ya kusalia nyumbani.

Maandamano hayo yamekuwa mtihani mkubwa kwa rais Buhari, ambaye ni afisa wa jeshi mstaafu aliyeingia madarakani kufuatia ushindi wa urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015 na ambaye sasa ni Kamanda Mkuu wa jeshi.

Maandamano hayo ndio makubwa zaidi kuwahi kutokea Nigeria tangu kumalizika kwa utawala wa kijeshi mwaka 1999.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG