Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliliambia baraza lake la mawaziri kwamba pendekezo la Wapalestina la kutaka kutambuliwa kwa taifa lao kwenye Umoja wa Mataifa wiki hii halitafaulu.
Aliwashutumu wapalestina kwa kukataa kurudi kwenye majadiliano ya moja kwa moja, ambayo anasema ndio njia pekee ya kupatikana amani.
Bw. Netanyahu alisema, Israel inashirikiana kwa karibu na Marekani kuhakikisha kuwa Baraza la Usalama litakataa ombi hilo la wapalestina kutaka kukubaliwa kwenye Umoja wa Mataifa kama mwanachama kamili. Marekani imetishia kutumia kura yake ya turufu, ikisema hatua za upande mmoja hazibuni kitu na ikawahimiza wapalestina kurejea kwenye meza ya majadiliano.
Wapalestina wameweka masharti ya kurejea kwenye majadiliano, wakisema watafanya hivyo tu iwapo Israel itasitisha upanuzi wa makazi ya walowezi huko ukanda wa Magharibi na Jerusalem Mashariki. Israel imekataa masharti hayo.
Utawala wa Marekani nao pia unapinga shughuli hizo za ujenzi wa makazi. Kutokana na msimamo huo, afisa wa kipalestina Nabil Shaath, anashangazwa na kwanini Marekani basi inapinga kulitambua taifa la kipalestina. Alizungumza kwenye redio ya kijeshi ya Israel.
“Sioni kwanini wamarekani watatuadhibu kwa sisi kwenda kwenye Umoja wa Mataifa, pale wao hawawezi hata kuwazuiwya waisraili kusitisha ujenzi wa makazi ya walowezi, hawawezi kufanya hatua thabiti za kurejea kwenye majadiliano. Sifahamu kwa nini wanatuadhibu.”
Waziri mkuu Netanyahu na rais wa Palestina Mahmoud Abbass watalihotubia Baraza Kuu la Umoja Mataifa siku ya ijumaa. Baadae Bw. Abbass atawasilisha ombi la Palestina kutambuliwa kuwa taifa kwa Baraza la Usalama.