Trump anatarajiwa kuwafahamisha kwa kina mpango uliokuwa unangojewa kwa muda mrefu katika kutafuta suluhu ya mgogoro wa Israeli na Wapalestina.
Mpango huo unatarajiwa kuzinduliwa kwa umma siku ya Jumanne wakati wa mkutano wa pamoja kati ya Trump na Netanyahu na waandishi wa habari.
“Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita nilikuwa nimefanya mazungumzo mengi na Rais Trump – rafiki mkubwa wa Israeli – na pia na timu yake juu ya masuala haya yenye maslahi muhimu, juu ya usalama wetu, na haki zetu,” Netanyahu amesema Jumapili.
“Kesho nitakutana na Rais Trump na Jumanne, sote kwa pamoja, tutaandika historia.
Gantz amesema yeye anasubiria kwa hamu kwa kile alichokiita “ni ziara muhimu sana.”
“Mpango wa mkutano huo ni kushughulikia usalama wa Israeli, mikakati ya kieneo – na kuna matumaini ya kupatikana utulivu katika kufikia hilo,” amesema.
Lakini Wapalestina wamepinga mwenendo wa uongozi wa Trump na kile wanachokiona ni upendeleo kwa Waisraeli, na mafanikio hayaonekani kabisa.
Wizara ya mambo ya nje ya Palestina imesema katika tamko Jumapili kuwa hakuna Mpalestina atakaye kubali mpango huo.
Trump amekuwa akihamasisha suala hilo kama ni "mpango wa karne" wakati undani wa mpango huo ukiwa siri katika kipindi chote cha miaka mitatu ya maandalizi yake.
Trump aliwakasirisha Wapalestina kutokana na hatua kadhaa alizochukuwa katika uongozi wake, ikiwemo kwenda kinyume na sera ya miongo mingi ya Marekani kwa kuitambua Jerusalem kuwa makao makuu ya Israeli na kuhamisha ubalozi wa Marekani huko.
Mikutano ya Ikulu ya Marekani inafanyika wakati Trump akikabiliwa na kesi ya kutaka kumuondoa madarakani, na bunge la Israeli likitafakari ombi la Netanyahu kupewa kinga ya kutofunguliwa mashtaka ya ufisadi, na viongozi hao wawili wa Israeli wakijiandaa kushiriki katika uchaguzi mkuu Machi 2, 2020.