Amesema kuwa Marekani itapohamisha ubalozi wake Jerusalem nchi nyingine zitafanya hivyo pia.
Netanyahu amesema nchi yake inaendelea kuwasiliana na mataifa mengine lakini hakuzitaja nchi hizo, wakati akitoa hotuba yake katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Israel.
Jeshi la Israel limetangaza kuongeza vikosi zaidi kwenye Ukingo wa Magharibi ikiwa ni sehemu ya kile walichokiita “kuwa tayari kukabiliana na matukio yoyote.”
Uamuzi wa Rais wa Marekani Donald Trump kubadilisha sera ya Marekani ya miongo mingi juu ya suala la Jerusalem na kuanzisha harakati za mchakato wa kuhamisha ubalozi wa Marekani kutoka Tel Aviv umepingwa vikali na viongozi wa Palestina.
Rais wa Palestina Mahmoud Abbas amesema mpango wa Trump umeifanya Marekani kupoteza nafasi yake ya usuluhishi katika kutafuta amani.
Kiongozi wa Hamas Ismail Haniyeh ametaka kuwepo kwa mandamano ya Wapalestina yanayojulikana kama intifada, au muamko wa kupinga Israel kuanzia Ijumaa.
“Tunataka maadamano haya yadumu na kuendelea ili kumfanya Trump na wanaokalia ardhi ya Palestina wajute kwa kufanya uamuzi huu,” Haniyeh amesema Alhamisi alipokuwa anatoa hotuba huko Gaza.