Hatua hiyo imechukuliwa mapema hii Ijumaa na Kamati ya Maadili ya Taifa ya Tume ya Uchaguzi.
Katika taarifa yake, kamati hiyo ikisema imechukuwa hatua hiyo kutokana na malalamiko yaliyowasilishwa na Chama cha NRA na CCM.
Vyama hivyo vinamlalamikia Lissu kutokana na kauli aliyoitoa mkoani Mara alipodai kuwa Magufuli aliitisha kikao cha wasimamizi wa uchaguzi nchi nzima kuhujumu uchaguzi.
Pia wamedai vyama hivyo vimelalamika kuwa Lissu alitoa kauli za kichochezi kila alipokuwa akifanya kampeni mkoani Geita.
"Baada ya makubaliano ya kina kamati imekubali kuwa Tundu Lissu amekiuka maadili ya uchaguzi kwa kutoa lugha chochezi na tuhuma zisizothibitika kinyume cha kanuni," taarifa imeeleza.
Naye Lissu amesema uamuzi huo sio wa haki akiongeza kwamba kabla ya kupatiwa adhabu anatakiwa kuelezewa tuhuma zake.
''Taratibu zote zilizowekwa katika maadili ya uchaguzi zimevurugwa', alisema mwanasiasa huyo.
Tume ya Taifa ya Uchaguzi Tanzania imesema anaruhusiwa kukata rufaa.