Makamu Mwenyekiti wa NEC, Jaji Mbarouk Salim Mbarouk, alisema uchaguzi huo umetangazwa baada ya kupokea barua kutoka kwa Spika wa Bunge, Job Ndugai ambayo iliainisha majimbo matatu yaliyo wazi.
“Barua ya Spika imeandikwa kwa kuzingatia kifungu cha 37(3) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, ambayo inamtaka kuitaarifu tume uwepo wa nafasi wazi za ubunge katika majimbo ambayo hayana wabunge kutokana na sababu mbalimbali,” alisema Jaji Mbarouk.
Alisema Jimbo la Korogwe Vijijini mkoani Tanga lilibaki wazi baada ya kifo cha aliyekuwa Mbunge wake Stephen Ngonyani kilichotokea Julai 2, mwaka huu.
Jaji Mbarouk alisema Jimbo la Ukonga jijini Dar es Salaam litafanya uchaguzi baada ya aliyekuwa Mbunge wake, Mwita Waitara kujivua uanachama wa Chadema Julai 29, mwaka huu na kuhamia CCM, hivyo kupoteza sifa ya kuwa mbunge, gazeti la Mtanzania limeripoti.
Kama ilivyotokea Ukonga, Jimbo la Monduli lililopo mkoani Arusha nalo litafanya uchaguzi baada ya aliyekuwa mbunge wake, Julius Kalanga kujivua uanachama wa Chadema na kuhamia CCM Julai 31, mwaka huu na hivyo naye kupoteza sifa ya kuwa mbunge.
“Baada ya kupokea taarifa hizo na kwa mujibu wa vifungu vya 37 (1) (b) na 46 (2) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, NEC inatoa taarifa kwa umma kuwa majimbo matatu ya Korogwe Vijijini, Ukonga na Monduli yapo wazi,” alisema Jaji Mbarouk.
Alisema kutokana na hilo, NEC itaendesha zoezi la uchukuaji fomu za uteuzi kuanzia Agosti 31 hadi 20, mwaka huu.
Jaji Mbarouk alisema ratiba ya uchaguzi huo ilitolewa kwa kuzingatia masharti ya vifungu vya 37(1)(b) (5) na 46 (2) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi.
Pamoja na hayo, Jaji Mbarouk alisema kampeni na uchaguzi wa madiwani kwa kata za Tindabuligi na Kisesa katika Halmashauri ya Wilaya ya Meatu ambazo ziliahirishwa hapo awali, zitaendelea na uchaguzi utafanyika sambamba na ratiba iliyotajwa katika majimbo hayo matatu.
"Tume inachukua nafasi hii kuvikumbusha vyama vya siasa na wadau wote wa uchaguzi kuzingatia sheria, kanuni, taratibu, miongozo na maelekezo yote wakati wa kipindi cha uchaguzi mdogo wa majimbo hayo matatu na hizo kata mbili,” alisema Jaji Mbarouk.
Ratiba hiyo imetolewa wakati vyama vikiwa katika kampeni za uchaguzi wa ubunge katika Jimbo la Buyungu mkoani Kigoma pamoja na kata 77 utakaofanyika Agosti 12.