Mapigano makali yalianza Jumatatu, wanajeshi wa serikali wakilenga kuchukua tena mji huo kutoka kwa waasi.
Wanajeshi wa DRC wanatumia silaha nzito zikiwemo mabomu kuwashambulia waasi hao.
Jeshi la DRC linatumia ndege zilizotengenezwa Russia, aina ya Sukhoi-25 kushambulia waasi wa M23. Kulingana na mwandishi wetu wa DRC, waasi wa M23 wamejaribu kupiga ndege hizo kwa risasi bila mafanikio.
Serikali ya DRC inasisitiza kwamba waasi wa M23 wanaungwa mkono na serikali ya Rwanda.
Rais wa Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo Felix Tshisekedi ametaka “Umoja wa mataifa kuwawekea vikwazo maafisa wa serikali ya Rwanda na makamanda wa ngazi ya juu wa kundi la M23.”
Kundi la M23 linaongozwa na Generali Sultan Makenga.
Rwanda ilijaribu kuangusha ndege ya vita ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo wiki iliyopita, ikidai kwamba ndege hiyo ilikuwa imeingia katika anga yake. DRC ilifutilia mbali madai hayo ikiishutumu Rwanda kwa kutaka kuanzisha vita, na kusema kwamba ndege iliyopigwa kombora na Rwanda, ilikuwa inajitayarisha kutua katika uwanja wa ndege wa kimataifa wa Goma.
Ndege za kivita za Sukhoi-25 zinazotumiwa na DRC kushambulia waasi wa M23, zina uwezo mkubwa wa kutekeleza mashambulizi wakati wowote, iwe usiku au mchana hata katika hali mbaya ya hewa.
Kuharibika kwa diplomasia kati ya DRC na Rwanda
Mgogoro kati ya Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo na Jirani yake Rwanda, umekuwa ukiharibika kila siku tangu mwaka 2021, wakati waasi wa M23 walipoanzisha vita na kudhibithi mji wa Bunagana, karibu na Uganda.
Rwanda inadai kwamba Jamhuri ya kidemokrasia ya Congo inaunga mkono waasi wa FDLR wenye nia ya kupindua serikali ya rais Paul Kagame.
Mashambulizi yanayotekelezwa na ndege za kivita yanafuatiwa na mashambulizi ya wanajeshi wa ardhini ambao wanaripotiwa kudhibithi sehemu za Kitobo, Mungote na Kilolirwe wakilenga kuwafurusha waasi wa M23 kutoka Kitchanga.
Mabomu yanaendelea kuanguka Kitchanga huku rais Tshisekedi akiwa amewaambia wanadiplomasia walio Kinshasa kwamba “DRC italinda mipaka yake kwa njia zote kwa gharama zote na hakuna sehemu ya nchi hiyo itachukuliwa na Rwanda.”
DRC na Rwanda zimeshutumiana kila mara na kuvunja makubaliano ya kuleta amani ya jumuiya ya Afrika mashariki na Angola.
Mapigano hayo yamesababisha maelfu ya raia wa Congo kukimbilia Rwanda na Uganda kama wakimbizi.