Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 19:54

Nchi za Umoja wa Afrika zaanza kutambua mchango wa mahakama ya Afrika ya haki za binadamu


Ramani ya mkoa wa Arusha
Ramani ya mkoa wa Arusha

Nchi za Umoja wa Afrika zimeanza kutambua mchango wa mahakama ya Afrika ya haki za binadamu yenye makao yake makuu Arusha Kaskazini mwa Tanzania , ikiwemo upatikanaji wa haki, kuimarisha demokrasia na kuchochea ukuaji wa uchumi, rais wa mahakama hiyo amesema Jumatatu.

Mahakama ya afrika ya haki za binadamu iliyoanzishwa na nchi za umoja wa Afrika kwa lengo la kusimamia haki za binadamu mwaka 2006 mjini Addisa Ababa, Ethiopia ilihamishia shughuli zake Arusha Tanzania Mwaka 2007.

katika utekelezaji wa majukumu yake kwa muda mrefu sasa imekuwa ikikabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo ya asilimia kubwa ya nchi kuridhia itifaki ya kuanzisha mahakama hiyo, lakini kupata kigugumizi cha kutoa tamko la kuwaruhusu wananchi na taasisi za kiraia kupeleka mashauri yake moja kwa moja kwenye mahakama hiyo.

Hata hivyo , Rais wa mahakama hiyo Jaji Iman Aboud amesema kwa sasa tatizo hilo limeanza kuonyesha mwelekeo wa kupata ufumbuzi, baada ya nchi nyingi za Umoja wa Afrika kuanza kutambua mchango wa mahakama hiyo katika masuala mbalimbali yakiwemo ya kusimamia haki, demokrasia na pia kuimarisha misingi ya kiuchumi.

Jaji Aboud amesema baadhi ya nchi ambazo zilikuwa bado hazijatoa tamko la kuwaruhusu Wanainchi wake kutumia mahakama hiyo ziko kwenye mchakato wa kuondoa kikwazo hicho , hatua ambayo ni matokeo ya uhamasishaji unaoendelea wa kuelezea kazi nzuri inayofanywa na mahakama hiyo.

“Nchi mbalimbali zimeelewa umuhimu wa mahakama na kazi zake. Tumekwenda Zambia, tumekwenda Mauritania, tumefanya mazungumzo na viongozi wa serikali wametuahidi kuwa wako tayari kuridhia wananchi wote kuleta mashauri yao mahakamani, na tutaendelea kwenda nchi nyingine kufanya mazungumzo na viongozi, kwani nchi nyingi sio kama hawataki bali hawajaelewa sawa,” amesema Jaji Aboud.

Kwa mujibu wa Jaji Aboud pia mahakama inaendelea na mazungumzo na baadhi ya nchi zilizokuwa zimetoa tamko la kuwaruhusu wananchi wake kupeleka mashauri kwenye mahakama hiyo na baadaye kuliondoa ikiwemo Tanzania.

"Tunategemea Tanzania kama mwenyeji wa mahakama hii , itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kuona tena inarejea kuwa moja ya nchi ambazo zinaruhusu wananchi wao kuleta mashauri yao mahakamani kama ilivyokuwa awali,” amesema.

Kati ya nchi 55 za umoja wa afrika ni nchi 33 zilizoridhia itifaki ya kuanzishwa kwa mahakama hiyo ambapo kati ya hizo, ni nchi 8 tu zilizotoa tamko la kuwaruhusu wananchi wake na taasisi za kiraia kupeleka mashauri yao moja kwa moja katika mahakama hiyo.

Ripoti hii imeandaliwa na mwandishi wetu wa Arusha, Asiraji Mvungi

XS
SM
MD
LG