Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 22:20

Nani wanahusika na mapigano yasiyomalizika DRC?


Wapiganaji wakiwa wamebebea silaha katika mji wa Goma, mashariki mwa DRC
Wapiganaji wakiwa wamebebea silaha katika mji wa Goma, mashariki mwa DRC

Milio ya risasi iliposikika, Dansira Karikumutima alianza kukimbia. “Nilikimbia na familia yangu. Kila mtu alikimbia kujiokoa.” Hii ilikuwa mwezi Machi mwaka huu 2022, waasi wa M23 waliposhambulia Kijiji cha Cheya, mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, jimbo la Kivu kaskazini.

Miezi 4 baadaye, Dansira mwenye umri wa miaka 52, na Watoto 11, wanaishi katika kambi ya wakimbizi, ambayo pia ni shule ya msingi mjini Rutshuru.

Wanalala shuleni humo, na mchana wanajitafutia chakula kwa kulima katika mashamba ya watu wanaoishi karibu na kambi hiyo.

Dansira na familia yake ni miongoni mwa idadi kubwa ya wakimbizi inayoendelea kuongezeka mashariki wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Ripoti ya shirika la maalum la uchunguzi Afrika inasema kwamba iwapo mzozo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo unatishia kuliingiza eneo la Maziwa Makuu katika mgogoro mkubwa wa kiusalama.

https://africacenter.org/spotlight/rwanda-drc-risk-of-war-new-m23-rebellion-emerges-explainer

Kundi la waasi la M23 ni miongoni mwa zaidi ya makundi 100 yanayopigana na serikali mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Karibu watu 8,000 wamefariki tangu mwaka 2017 kutokana na mapigano mashariki mwa DRC kwa mujibu wa shirika linalofuatilia maswala ya usalama eneo la Kivu.

(( https://kivusecurity.org/ ))

Umoja wa Mataifa umesema kwamba zaidi ya watu milioni 5.5 wamekoseshwa makao – 700,000 mwaka huu.

Baraza linaloshughulikia wakimbizi nchini Norway limeitaja DRC kuwa nchi ambayo hazingatiwi sana na kutiliwa maanani licha ya kuwa na idadi kubwa ya wakimbizi wa ndani.

(( https://www.nrc.no/news/2022/june/the-worlds-ten-most-neglected-crises-are-all-in-africa/ ))

Mapigano ya DRC yanachangiwa na sababu kadhaa zikiwemo siasa za kanda hiyo, ukabila, uhasama ndani ya nchi, na ushindani wa kudhibithi utajiri mkubwa wa rasilimali za nchi.

Mapigano hayo yamesababisha uhasama kati ya DRC na Jirani yake, Rwanda, ambayo bado inauguza vidonda vya mauaji ya kimbari ya mwaka 1994 ambapo watu kutoka kabila la Wahutu waliwaua karibu Watutsi 800,000 na baadhi ya wahutu.

Mgogoro wa DRC vile vile umefufua uhasama wa muda mrefu kati ya Rwanda na Uganda.

Kundi la M23 linajihusha kwa njia gani kwenye uhasama baina ya DRC na Rwanda

DRC na rais wake Felix Tshisekedi, inaishutumu Rwanda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23.

Miongoni mwa wapiganaji wa M23 ni watu kutoka kabila la Watutsi.

M23 ni kundi lilioanzishwa mwezi Machi mwaka 2009 baada ya kufeli kwa mkataba wa amani kati ya waasi waliotoroka katika jeshi la taifa na serikali ya DRC. Kundi hilo la waasi lilikuwa limeudhibithi mji wa Goma mwaka 2012.

Lilizidiwa nguvu na wanajeshi wa Umoja wa Mataifa MONUSCO na kuondoka Goma.

Rwanda na rais wake, Paul Kagame, inaishutumu DRC kwa kuwaunga mkono waasi wa Democratic Forces for the Liberation of Rwanda FDLR, ambalo ni kundi lililo nchini Congo na linalojumulisha wapiganaji kutoka kabila la Wahutu, wanaoshutumiwa na Rwanda kwa kusababisha mauaji ya kimbari mwaka 1994.

Nini kimesababisha waasi wa M23 kuongeza mashambulizi?

Mnamo mwezi Novemba mwaka uliopita, kundi la M23 lilishambulia kambi kadhaa za jeshi la DRC katika sehemu za Kivu Kaskazini, karibu na mpaka wa DRC, Uganda na Rwanda.

Waasi hao walidhibithi sehemu kadhaa ikiwemo kuwashinda nguvu wanajeshi wa DRC mnamo mwezi Mei na kudhibithi mji muhimu wa biashara kati ya DRC na Uganda wa Bunagana, mwezi Juni.

Bintou Keita, mkuu wa MONUSCO nchini DRC, alionya mnamo mwezi Juni kwamba kundi la M23 lilikuwa linaimarika kwa mashambulizi na kupata silaja nzito nzito na huenda likawa tishio kubwa sana kwa raia sehemu hiyo, na hata kuwazidi nguvu walinda usalama 16,000 wa Monusco.

(( https://www.voanews.com/a/un-well-armed-m23-rebels-resurgent-in-drc/6638775.html ))

Kundi la M23 lilianzisha mashambulizi likiwa na lengo la kuitaka serikali ya DRC kutekeleza mkataba.

(( https://www.csis.org/events/addressing-rising-tensions-between-drc-and-rwanda ))

Waasi hao wanataka mkataba wa mwaka 2013 uliosainiwa jijini Nairobi, Kenya, kutekelezwa. Mkataba huo utawasamehe kwamakosa yote ambayo wamefanya na kuwajumuisha katika jeshi la taifa, au kuruhusiwa kuishi maisha ya kawaida kama raia.

Je, mbona Uganda inatajwa kila mara katika mgogoro huu?

“Uhasama wa muda mrefu kati ya Uganda na Rwanda unatajwa kuwa sababu zinazofanya kundi la M23 kuimarisha mashambulizi.” Inasema ripoti ya utafiti ya Africa Center.

(( https://africacenter.org/spotlight/rwanda-drc-risk-of-war-new-m23-rebellion-emerges-explainer/ ))

Ripoti hiyo inasema kwamba “kuna hali ya kutoaminiana kati ya DRC na majirani zake Uganda, Rwanda na Burundi. Nchi hizo zote kwa jumla, pia haziaminiani.”

Mwishoni mwa mwezi Novemba mwaka uliopita, Uganda ilianzisha operesheni maalum dhidi ya kundi la waasi la Allied Democratic Forces - ADF, Kivu Kaskazini. Kundi hilo linaaminika kuwa na uhusiano na kundi la kigaidi la Islamic State na serikali ya Marekani imelitaja kuwa kundi la kigaidi.

Rais wa Uganda Yoweri Museveni amelishutumu kundi la ADF kwa kutekeleza mashambulizi ya mabomu jijini Kampala, mwezi Oktoba na Novemba mwaka uliopita.

Maafisa wa Uganda wameishutumu Rwanda kwa kulitumia kundi la M23 kuzuia operesheni dhidi ya kundi la ADF, kulingana na ripoti ya Africa Center, inayoongezea kwamba Umoja wa Mataifa pia “umeitaja Uganda kwa kuwaunga mkono waasi wa M23.

Uchunguzi uliofanywa na Umoja wa Mataifa unasema kwamba kuna ‘ushahidi wa kutosha kwamba Rwanda inahusika na mgogoro huo.”

Ripoti ya utafiti wa kundi la Congo Research Group, unasema kwamba “siasa za kanda zimepelekea mgogoro mkubwa mashariki mwa DRC,” Rwanda ikilalamika kwamba hatua ya Uganda kuingia sehemu hiyo kijeshi “inavuruga” maslahi yake mashariki mwa DRC.

Maslahi gani ya kiuchumi yanapelekea mgogoro huo?

Mapigano mashariki mwa DRC yanahusu utajiri wa madini ulio sehemu hiyo ikiwemo almasi, dhahabu, na mbao.

DRC ina utajiri mkubwa wa madini mengine kama Cobalt na Coltan, yanayotumika kutengeneza betri za gari na za simu za mkononi, miongoni mwa vifaa vingine vya elektroniki na vinavyotumika kutengeneza ndege.

“DRC huzalisha asilimia 70 ya madini ya Cobalt kote duniani na asilimia 60 ya Coltan.” Hii ni kulingana na ripoti ya uchimbaji madini ya Congo. Ripoti hiyo iliandikwa mwezi Februari. Ilieleza kwamba huenda DRC ikawa mtengenezaji mkubwa wa magari ya kutumia umeme.

(( https://www.mining-technology.com/analysis/kinshasa-africa-democratic-republic-congo-cobal /#:~:text=The%20DRC%20produces%20more%20than,calling%20the%20%22new%20oil%22. ))

Ripoti ya Africa Center inaeleza kwamba “kuna ushahidi wa kutosha kwamba waasi wenye uhusiano pamoja na Rwanda, wakiwemo wa M23 wanadhibithi biashara ya madini kutoka Kivu hadi Uganda na Rwanda.”

Ripoti hiyo inasema kwamba waasi hao wanatumia pesa kutokana na mauzo ya madini hayo kununua “silaha, kusajili wapiganaji na kudhibithi migodi pamoja na kuwalipa kwa njia za ufisadi maafisa wa forodha, wanajeshi na polisi.”

Usafirishaji wa madini hayo limekuwa jambo rahisi.

Mnamo mwaka 2019, DRC ilisaini makataba na Burundi pamoja na Tanzania, kujenga reli kutoka Tanzania hadi DRC kupitia Burundi, na hivyo kufanya iwe rahisi sana Burundi na DRC kusafirisha bidhaa zake hadi kwenye bandari ya Dar-es-salaam, bahari ya hindi.

Mwezi Juni mwaka 2021, Rais wa DRC Felix Tshisekedi alizindua ujenzi wa barabara akiwa na rais wa Uganda Yoweri Museveni. Barabara hiyo inaunganisha DRC na Uganda.

Gazeti la the East African liliripoti kwamba mradi huo unalenga kuimarisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

(( https://www.theeastafrican.co.ke/tea/news/east-africa/uganda-drc-decide-to-make-roads-not-war--2507976 ))

Mradi huo unahusisha ujenzi wa barabara kutoka bandari ya Goma kenye ziwa Kivu hadi mji wa Bunagana, mpaka wa DRC na Uganda.

“Rwanda, inaona haya yote yakifanyika na inahisi kwamba inatengwa.” Imesema ripoti ya Africa Center.

Rwanda imekuwa na mikataba kadhaa na serikali ya DRC, ikiwemo usafiri kwa kutumia shirika la ndege la Rwanda Air na mikataba kadhaa inayohusu madini. Serikali ya DRC imesitisha mikataba hiyo yote mnamo mwezi Juni.

Nini kinahitajika kumaliza mgogoro huu?

DRC ilijiunga rasmi na jumuiya ya Afrika Mashariki mwezi Juni mwaka huu.

Mataifa ya jumuiya ya Afrika Mashariki yalikubaliana kutuma jeshi la pamoja mashariki mwa DRC kupambana na makundi ya waasi.

Hakuna tarehe maalum imetangazwa kuhusu jeshi hilo litakapoingia DRC.

Tshisekedi, mwenye umri wa miaka 59, ambaye anajitayarisha kwa uchaguzi mkuu mwaka ujao 2023, amesema kwamba Rwanda haitaruhusiwa kuwa sehemu ya jeshi hilo la jumuiya ya Afrika Mashariki.

Rais wa Rwanda Paul Kagame, mwenye umri wa miaka 64, amesema “hana shida na hilo.”

https://www.voaswahili.com/a/kagame-hatujaomba-mtu-yeyote-kwamba-tupeleke-wanajeshi-wa-rwanda-drc/6645778.html

Viongozi hao wawili walikutana nchini Angola Juni tarehe 6 kwa mazungumzo yenye lengo la “kupunguza uhasama” kuhusiana na mapigano ya waasi nchini DRC.

Mkutano wa Angola ulikubaliana kwamba viongozi hao wapunguze uhasama na kwamba kundi la M23 liondoke mashariki mwa DRC haraka iwezekanavyo.

Lakini mapigano yalizuka kati ya M23 na wanasjeshi wa serikali saa chache baada ya makubaliano ya Angola, katika sehemu za Rutshuru, Kivu Kaskazini.

https://www.voaswahili.com/a/mapigano-makali-yanaendelea-kati-ya-wanajeshi-wa-drc-na-waasi-wa-m23-licha-ya-makubaliano-ya-angola/6648872.html

Msemaji wa kundi la M23 Meja Willy Ngoma, aliiambia idhaa ya Kiswahili ya VOA, katika kipindi cha Kwa Undani, kwamba kundi hilo haliwezi kutambua kikao cha Angola.

“Sisi tulisaini mkataba na bwana Tshisekedi na serikali ya Congo. Na tupo tayari kufanya mazungumzo. Yote wanayosema kwamba tuache mapigano na tuondoke DRC, wanataka twende wapi? Sisi ni raia wa Congo. Hatuwezi kwenda uhamishoni tena. Tunapigania haki zetu kama raia wa Congo.”

Serikali ya DRC inasema kwamba inataka waasi wa M23 kuondoka nchini humo ndipo mazungumzo yafanyike.

Paul Nantulya, wa kituo cha utafiti cha Africa Center, ametabiri kwamba “itachukua muda kutatua mgogoro kati ya Rwanda na DRC.”

Katika barua pepe aliyoituma VOA, Paul amependekeza ziwepo juhudi za upatanishi “kwa njia ya wazi, zinazoweza kutekelezwa kati ya Congo na majirani zake, ikianza na Rwanda, na ziwepo juhudi za kulileta pamoja taifa la Congo kisiasa.”

Balozi wa Rwanda nchini DRC Vincent Karega, katika mahojiano na idhaa ya Afrika ya Kati ya Sauti ya Amerika VOA, mwezi Juni, alisema kwamba ujumbe wa chuki umeenea mashariki mwa Congo dhidi ya jamii ya Wanyarwanda wanaoishi nchini humo na kuonya kwamba huenda machafuko yakatokea, na kutaka “dunia nzima kuingilia kati kuhakikisha kwamba mapigano mabaya hayatokei.”

Ripoti hii imeandaliwa na Kennes Bwire VOA Swahili Service (( https://www.voaswahili.com/ )); Mhariri wa divisheni ya matangazo ya VOA kuelekea Afrika Carol Guensburg. Wengine waliochangia ni Etienne Karekezi, Geoffrey Mutagoma na Venuste Nshimiyimana wa idhaa ya Afrika ya kati ya VOA Austere Malivika wa idhaa ya kiswahili na mwandishi maalum wa VOA kutoka makao makuu ya umoja wa mataifa Margaret Besheer,

XS
SM
MD
LG