Baraza la utawala nchini Sudan lilikubali kujiuzulu kwa mwendesha mashtaka wa umma na kumwondoa mkuu wa mahakama katika wadhifa wake, taarifa ya baraza hilo ilisema Jumatatu.
Hakuna sababu iliyotolewa juu ya uamuzi huo, ingawa taarifa hiyo ilisema kwamba Mwendesha Mashtaka wa Umma Tajalsir al-Hibir aliomba mara kadhaa kuachia madaraka.
Baraza lilitoa tangazo hilo chini ya wiki moja baada ya waandamanaji wawili kuuawa kwenye maandamano ya kuadhimisha siku ya uvamizi mbaya katika eneo la maandamano wakati wa ghasia za 2019 zilizomuondoa madarakani rais wa zamani Omar al-Bashir.
Majibu ya mauaji hayo ya wiki iliyopita yanaonekana kama mtihani wa uhusiano tete kati ya mamlaka ya raia na ya kijeshi ambao sasa wanashirikiana madaraka.
Baada ya hayo kutokea, baraza la mawaziri la mpito la kiraia la Sudan lililalamikia ucheleweshaji wa kuwafikisha mahakamani wahusika wa uvamizi wa mwaka 2019 na matukio mengine yanayohusishwa na wafuasi wa utawala wa zamani.