Mahakama kuu ya Sudan Kusini mjini Juba siku ya Jumanne ilimhukumu mwanaharakati wa kutetea amani na mchumi maarufu nchini humo Peter Biar Ajak kwa kifungo cha miaka miwili jela baada ya kushutumiwa kuchochea ghasia akiwa katika jela maarufu ya Blue House inayojulikana kufunga watu waliotenda makosa mabaya. Nyathon Hotmai, mke wa mwanaharakati huyo alianza kulia pale jaji Sumaiya Saleh Abdallah alipotangaza hukumu hiyo.
Jaji Sumaiya Saleh Abdallah alieleza kwamba Ajak alikiuka vipengele kadhaa vya hati ya kanuni za uhalifu Sudan Kusini na alimhukumu kwa kuvuruga amani kwa sababu alifanya mahojiano na vyombo vya habari vya kigeni baada ya kukamatwa kwake kwa mashtaka ya uhaini ambayo baadae yalifutwa.
Wakati huo huo mfanyabiashara mhisani mkuu wa Sudan Kusini, Kerbino Wol alihukumiwa kifungo cha miaka 13 kwa shutuma za kuongoza uasi. Watu wengine wane walihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela. Hata hivyo wanasheria wa Ajak na Wol walidhamiria kukata rufaa kutokana na hukumu hiyo dhidi ya wateja wao.
Philip Anyang mwanasheria wa Ajak alieleza kwamba mteja wake alipata matatizo kwa kuzungumza na Sauti ya Amerika-VOA wakati wa uasi huo .
Anyang akizungumza na kipindi cha South Sudan in Focus cha VOA alieleza kwamba mahakama ilikwepa misingi ya sheria. Alisema Peter alikuwa anajieleza kwanza kwa sababu anashtakiwa kwa kuzungumza na VOA. Na kama hiyo ni kesi dhidi yake basi haki ya uhuru wa kuzungumza inahujumiwa Sudan Kusini.
Jaji Abdallah alieleza kwamba mahojiano ya Ajak na VOA yaliyofanyika Oktoba mwaka jana wakati wa uasi kwenye makao makuu ya usalama wa taifa yanayofahamika pia kama Blue House yalisababisha ghasia.
Ajak mwenye miaka 34 alikuwa akifanya kazi kama mchumi katika benki ya Dunia na alikamatwa Julai mwaka jana baada ya kuwakosowa viongozi wa serikali na upinzani huko Sudan Kusini kwa kushindwa kumaliza miaka mitano ya mgogoro wa kisiasa nchini humo.