Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 17:53

Museveni, Kagame waahidi kuendeleza ushirikiano


Rais Paul Kagame (kushoto) and Rais Yoweri Museveni
Rais Paul Kagame (kushoto) and Rais Yoweri Museveni

Rais wa Rwanda Paul Kagame amekutana na mwenzake wa Uganda Yoweri Museveni, huku kukiwa na ripoti za kuwepo uhusiano mbaya wa kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili.

Katika kikao na waandishi wa habari, Viongozi hao wawili wameeleza kwamba wanashirikiana katika kuendeleza agenda ya maendeleo na usalama katika nchi za maziwa makuu.

Mkutano wao mfupi, umefanyika siku tatu baada ya kikao cha Marais wa Bara la Africa kukutana mjini kigali , Rwanda kilichokubaliana kushirikiana kibiashara. Museveni hakuhudhuria kikao hicho.

"Tumekubaliana kushirikiana katika ujenzi wa reli ya kisasa, usambasaji wa umeme, ushirikiano katika safari za ndege na usalama kati ya Rwanda na Uganda, na pia nchi jirani" amesema Rais wa Uganda Yoweri Museveni baada ya kikao na mgeni wake.

Viongozi hao wamekiri kwamba kumekuwepo ukosefu wa kuelewana kati ya maafisa wa Rwanda na Uganda, lakini Museveni akawa mwepesi kuwalaumu mawaziri katika nchi zote mbili kwa kukosa kuwasiliana.

"Waziri wa Rwanda, anaona ni vigumu sana kumpigia simu waziri mwenzake wa Uganda. Yapo mambo ambayo yanaweza kusuluhishwa kwa simu," amesema Museveni.

Rais Kagame ameonekana sana kupima matamshi anayotoa, akimwachia mwenyeji wake kuzungumza zaidi lakini akasisitiza kwamba ni matumaimi yake kwamba mikutano inastahili kuleta maelewano ya kisumu.

Lakini museveni akasisitiza kwamba wamekubaliana kushirikiana katika ujasusi ili kusuluhisha tetesi za Rwanda kwamba raia wake wanakamatwa nchini Uganda.

"Kuna mambo madogo sana kati ya Rwanda na Uganda. Uganda ina matatizo ya mpaka na Tanzania, Jamhuri ya kidemokrasia ya kongo, na Kenya kuhusu kisiwa cha Migingo. Lakini haya ya Rwanda ni madogo sana. Tutayasuluhisha," amesisitiza Museveni.

Viongozi hao vilevile wanataka juhudi za haraka kuchukuliwa ili kuleta hali ya utulivu nchini Jamhuri ya kidemokrasia ya Kongo, Museveni akisema kwamba idadi ya wakimbizi wanaoingia Uganda kutoka Kongo ni ya kutisha na kuongeza kwamba Umoja wa Mataifa unastahili kuchukua hatua kuhakikisha kwamba mzozo wa Kongo unamalizika kwa haraka.

Mkutano kati ya Museveni na Kagame unaelezwa na wachambuzi wa siasa kuwa hatua nzuri ya kutatua changamoto za kidiplomasia kati ya nchi hizo mbili, zinazoletwa na hali ya kutoaminiana hasa baada ya Uganda kuwakamata watu kadhaa kutoka Rwanda kwa shutuma kwamba walikuwa ni majasusi waliotumwa na serikali ya Rwanda, kuwaangamiza maadui wa kisiasa.

Imetayarishwa na Mwandishi wetu Kennes Bwire, Washington, DC

XS
SM
MD
LG