Hatimaye, rais Robert Mugabe wa Zimbabwe amejiuzulu wadhifa huo Jumanne muda mfupi baada ya bunge la nchi hiyo kuanza utaratibu wa kumwondoa madarakani baada ya utawala wa miaka 37.
Kiongozi huyo mwenye umri wa miaka 93 amekuwa aking'ang'ania madaraka kwa wiki nzima baada ya jeshi kuchukua sehemu kubwa ya madaraka na chama chake mwenyewe cha ZANU-PF kumvua uongozi wa chama hicho.
Sherehe ziliibuka katika kikao cha pamoja cha bunge pale Spika Jacob Mudenda alipotangaza kuwa Mugabe amejiuzulu na hivyo kusimamisha utaratibu ulioanza wa kumwondoa madarakani.
Jeshi liliingilia kati mgogoro wa kisiasa nchini humo wiki iliyopita baada ya Mugabe kumfukuza kazi makamu rais Emmerson Mnangagwa ambaye alikuwa anatazamiwa kumrithi katika uongozi wa chama na urais. Hatua ya kumfukuza Mnangagwa ilionekana kama namna ya kufungua njia kwa mkewe wake Grace Mugabe hatimaye kuchukua uongozi wa nchi hiyo.
Mnangagwa, ambaye zamani alikuwa mkuu wa usalama na alishirikiana na Mugabe katika harakati za ukombozi wa nchi hiyo anatazamiwa kuchukua uongozi wa nchi.
Mamia ya wananchi wa Zimbabwe wamejitokeza katika mitaa ya miji mikubwa kama vile Harare kushangalia hatua ya Mugabe kujiuzulu, wakitazamiwa Zimbabwe mpya baada ya hapo.