Hosni Mubarak alifikishwa katika mahakama moja mjini Cairo Jumatano, akiwa kwenye kitanda cha hospitali na amekana mashtaka kwamba aliamrisha mauwaji ya mamia ya waandamanaji.
Baada ya kikao kifupi hakimu aliahirisha kesi hadi Agusti 15.
Vyombo vya habari kote duniani vilitangaza moja kwa moja kuanza kwa kesi hiyo ya kihistoria ya Bw. Mubarak mjini Cairo. Rais huyo wa zamani ambaye anashtakiwa pia kwa ulaji rushwa, ni kiongozi wa kwanza wa kiarabu kufikishwa mahakamani tangu kuzuka kwa wimbi la upinzani wa wananchi kote Afrika Kaskazini na Mashariki ya Kati mwaka huu.
Kote mjini Cairo, wamisri walikusanyika mbele ya televisheni zilizowekwa kwenye migahawa na majengo mbali mbali ili kushuhudia kiongozi wao wa miaka 30 akiwa kizimbani akiwa amevalia mavazi meupe na kulala kwenye kitanda akisikiliza kufunguliwa kesi yake.
Bw. Mubarak anatuhumiwa kwa kuamrisha mauwaji ya karibu watu 900 wakati wa siku 18 ya upinzani wa wananchi kutaka mageuzi ya kidemokrasia yaliyopelekea kujiuzulu kwake mwezi Febuari.Akipatikana na hatia huweza akahukumiwa kifo.