Shirika la afya duniani WHO, limetangaza kifo hicho, kufuatia mlipuko mpya wa Ebola nchini DRC.
Vipimo vya madaktari vimebaini kuwepo maambukizi ya ebola katika mji wa Mbandaka na kuna wasiwasi mkubwa kwamba huenda maambukizi yakasambaa hadi sehemu nyingine za nchi.
Maambukizi ya sasa yanaaminika kutoka kwa mnyama na wala sio kutokana na maambukizi ya awali kati ya binadamu.
Mtu aliyefariki ni mwanamke mwenye umri wa miaka 25, ambaye ana uhusiano wa kifamilia na mgonjwa wa kwanza ambaye pia alifariki.
Mgonjwa wa kwanza alianza kuonyesha dalili mnamo April tarehe 5 lakini hakutafuta matibabu kwa zaidi ya wiki moja. Alifariki April 21.
Maafisa wa afya wanaendelea kuwatafuta watu waliokaribiana na wawili hao waliofariki.
Karibu watu 145 waliokaribiana na wagonjwa, wanachunguzwa.
DRC imeshuhudia milipuko 13 ya Ebola, ikiwemo mlipuko wa mwaka 2018 hadi 2020, ambapo karibu watu 2,300 walifariki.