Maafisa wa serikali walisema watu 150 walijeruhiwa na mlipuko huo.
Mamlaka zilisema maafisa tisa wa polisi, ikiwa ni pamoja na naibu wa mkuu wa polisi mjini Addis Ababa, walikamatwa kuhusiana na tukio hilo.
Shirika la habari la BBC, liliripoti kwamba maafisa hao wa polisi wanafanyiwa uchunguzi "kwa kukosa kudhibiti eneo hilo la mkutano ambapo mlipuko huo ulitokea."
Waziri mkuu Abiy - ambaye kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters - ameleta mabadiliko makubwa ya kiutawala, alikuwa tu amemaliza kutoa hotuba yake wakati guruneti hiyo ilipolipuka.
Abiy alisema shambulizi hilo lilikuwa limepangwa na kwamba polisi wanachunguza ni nani aliyehusika.
Katika mahojiano ya televisheni Jumamosi, Abiy alisema upendo utashinda na kwamba kujaribu kuwaua watu si kuonyesha ushupavu.
"Wale waliojaribu kuwagawanya Waethiopia hawakufaulu," aliongeza.
Abiy alichukua usukani mwezi Aprili na amefanya mabadiliko mengi, ikiwa ni pamoja na kuwaachilia wafungwa wa kisiasa na waandishi wa habari.
Kadhalika ameanzisha mikakati ya uimarishaji wa uchumi huru na kuahidi kutafuta mwafaka wa amani kati ya Ethiopia na hasimu wake, Eritrea.