Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Novemba 05, 2024 Local time: 19:40

Mtu aiba ndege ya abiria na kuiangusha mjini Seattle, Marekani


Mfanyakazi mmoja kwenye uwanja wa Ndege mjini Seattle, jimbo la Washington, Marekani, Ijumaa jioni aliiba Ndege ya abiria na kupaa nayo kwa tariban saa moja, kabla ya kuiangusha kwenye kisiwa cha Ketron, kilicho karibu na uwanja huo wa Ndege.

Mkuu wa idara ya polisi katika Kaunti ya Pierce, aliandika ujumbe kupitia mtandao wa Twitter, na kueleza kwamba mtu huyo, mwenye umri wa miaka 29, aliigurumisha Ndege hiyo ya kampuni ya Horizon, muundo wa Q400, na baada ya kupaa bila mamlaka za uwanja wa Ndege kujua, akaanza kufanya michezo ya angani nayo.

Hata hivyo, ndege hiyo, iliyo na viti 76 vya abiria, haikuwa na abiria yeyote. Maafisa wa kuongoza safari za ndege walisikika wakimsihi mtu huyo atue, lakini akakaidi, huku akisema kuwa ana matatizo ya kibinafsi. Polisi wamemtaja mtu huyo kama aliyekuwa na nia ya kujiua.

Ndege iliyoanguka katika kisiwa cha Ketron baada ya kuibwa na mekanika wa shirika la ndege la Horizon.
Ndege iliyoanguka katika kisiwa cha Ketron baada ya kuibwa na mekanika wa shirika la ndege la Horizon.

Mawasiliano yaliyotolewa na kituo cha kuongoza safari za ndege mjini Seattle, yanaashiria kwamba mtu huyo alikuwa na nia ya kujitoa uhai.

"Ninajua kuna watu wengi wanaonipenda na nitawakosea kwa ninayotaka kuyafanya. Ningependa kuomba msamaha. Mimi ni mtu wa kawaida tu lakini nati na misumari iliyofunguka," alisema mtu huyo.

Punde tu baada ya Ndege hiyo kupaa, Ndege mbili za kivita aina ya F-15 za jeshi la Marekani, zilipaa na kuandamana nayo, katika juhudi za kutaka mtu huyo kutua salimini. Hata hivyo, Ndege hiyo ilianguka kwenye sehemu isiyo na wakazi wengi, na kusababisha moto mkubwa.

Shirika la habari la CNN liliripoti Jumamosi kwamba idara ya upelelelezi ya Marekani, FBI, imeanza kufanya uchunguzi wa kina kuhusiana na kisa hicho, huku wachambuzi wakkieleza wasiwasi wao kuhusu usalama kwenye viwanja vya ndege kufuatia tukio hilo la kipekee.

"Ni bahati kubwa kwamba ndege hiyo haikuwa na abiria. Kwa sasa tungekuwa tukizungumzia mkasa mkubwa zaidi. Hili ni jambo la kuchunguzwa kwa makini, hususan kwa sababu, tofauti na wahalifu wengine, mtu huyo alikuwa na kibali cha kuwa kwenye uwanja huo," alisema Justin Green, machambuzi wa masuala ya uchukuzi wa angani.

XS
SM
MD
LG