Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 08:37

Mtoto wa Museveni, anayeunga mkono Putin ‘kugombea’ Urais


Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni
Muhoozi Kainerugaba, mtoto wa rais wa Uganda Yoweri Museveni

Muhoozi Kainerugaba, mwanajeshi, kamanda wa jeshi la ardhini, mwanawe rais wa Uganda ambaye ametewala kwa mda mrefu, Yoweri Kaguta Museveni.

Ameonyesha waziwazi dalili za kutaka kumrithi babake kama rais wa Uganda, akiandika ujumbe kadhaa kuhusu maswala yanayoendelea kote duniani ikiwemo kuhusu vita vya Ethiopia na uvamizi wa Russia nchini Ukraine.

Ameandaa sherehe kuadhimisha kuzaliwa kwake ambazo zimeonekana kama mikutano ya kujipatia umaarufu wa kisiasa.

Endapo atagombea urais badala ya babake, katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2026, Muhoozi Kainerugaba atakabiliwa na ushindani mkali sana wa kisiasa kutoka kwa wapinzani wa sasa wa babake, wanaotaka kuzuia utawala wa kifamilia katika taifa hilo la Afrika mashariki.

Ushawishi wa kijeshi wa Muhoozi

Muhoozi amepokea mafunzo ya kijeshi nchini Uingereza katika chuo cha kijeshi cha Sandhurst Pamoja na nchini Marekani katika chuo cha mafunzo ya kijeshi cha Fort Leavenworth.

Kamanda huyo mwenye umri wa miaka 48 ana cheo cha lieutenant general. Japo wakosoaji wanasema amepandishwa cheo na babake kwa haraka sana katika mzingira ya kutatanisha.

Anaongoza kikosi cha jeshi la ardhini ambacho kinatambuliwa Uganda kama kinachoongoza jeshi lote la nchi hiyo.

Japo sheria ya Uganda inawazuia wanajeshi ambao hawajastaafu kujihusisha na siasa, Muhoozi ameahidi mabadiliko ya kisiasa na kujionyesha kama mtu anayejali maslahi ya vijana. Ameelezea nia yake kwa taifa.

"Wakati timu MK itakapochukua madaraka nchini humu, tutashinda! Tendo letu la kwanza litakuwa kuongeza bajeti ya wizara ya michezo!” aliandika Muhoozi kwenye twiter wakati wa sherehe za kuzaliwa kwake zilioandaliwa kote nchini humo.

Generali anayeandika sana maswala yenye utata kwenye twiter

Muhoozi amekuwa akiandika sana kwenye mitandao ya kijamii hasa twiter. Amejibizana na wanasiasa wa upinzani kuhusu maswala ya siasa.

"Putin yupo sahihi kabisa," aliandika Muhoozi siku chache baada ya rais wa Russia Vladmir Putin kuvamia Ukraine kijeshi licha ya ushirikiano mzuri wa mda mrefu kati ya Uganda na mataifa ya magharibi.

"Watu wengi ambao sio wazungu wanaunga mkono Russia kuivamia Ukraine.”

Ameunga mkono wapiganaji wa Tigray ambao wamekuwa wakipigana na serikali ya Ethiopia, na ametishia kuingilia mapinduzi ya kijeshi ya Guinea.

Juhudi za kujipatia umaarufu wa kisiasa

Kwa wiki kadhaa, ameandaa sherehe za kuzaliwa kwake zilizoanza Aprili 24. Wafuasi wa chama kinachotawala cha National resistance movement - NRM, waliandaa mikutano na hafla za kutoa misaada, wakiwa wamevalia fulana zenye picha ya Kainerugaba.

Alishiriki mbio za masafa marefu zilizoandaliwa jijini Kampala, Pamoja na hafla ya sherehe katika mji wa Entebbe, kwa heshima yake.

Siku ya kusherehekea kuzaliwa kwake, babake alimwandalia sherehe kubwa sana iliyohudhuriwa na rais wa Rwanda Paul Kagame na watu wengine maarufu nchini Uganda.

"Ukweli ni kwamba waliokuwa wakinitusi kila siku, wanalazimika sasa kumeza machungu ya maneno yao!!” Kainerugaba aliandika ujumbe wa twiter mapema mwezi huu.

Nguvu za jeshi la Uganda katika siasa za nchi hiyo

Jeshi la Uganda lina maamuzi makubwa sana katika siasa za Uganda na babake Muhoozi ametumia jeshi hilo kutawala nchi hiyo mwa mda mrefu Zaidi. Muhoozi anategemea jeshi hilo kumuunga mkono endapo babake ataamua kwamba anataka kuondoka madarakani.

“Ameishi katika ikulu ya rais tangu utotoni. Hiyo ni fursa kubwa kwake kuanza maisha ya uongozi wa nchi hiyo na kwa urahisi mkubwa ikilinganishwa na wanasiasa wengine. Kwa sababu hiyo, huwezi kumlinganisha na wanasiasa wengine,” amesema Moses Khisa, mchambuzi wa siasa za Uganda ambaye pia ni mhadhiri katika chuo kikuu cha jimbo la North Carolina.

Je, Muhoozi Kainerugaba ana sifa za kisiasa?

Wachambuzi wanamuona Kainerugaba kama mtu asiyekuwa na mvuto wa kisiasa kama babake.

Museveni aliongoza mapinduzi yaliyomuingiza madarakani mwaka 1986 na amekuwa akishinda uchaguzi mara sita, japo uchaguzi huo umetajwa kutokuwa huru na haki.

Wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakipigwa na kukamatwa katika msako mkali wa maafisa wa jeshi Pamoja na polisi.

"Hana uungwaji wa watu. Hawezi kushinda uchaguzi huru na haki,” amesema mchambuzi na mwanasheria nchini Uganda Gawaya Tegulle.

Utawala wa Museveni umekuwa ukimulikwa kwa ukandamizaji

Japo Museveni alisifiwa na mataifa ya magharibi katika vita dhidi ya wapiganaji wa kiislamu, umekumbwa na madai ya ukandamizaji wa raia, ghasia za kingono na mauaji yanayofanywa na maafisa wa usalama.

Marekani imewawekea vikwazo maafisa wa ngazi ya juu wa usalama wa Uganda akiwemo Maj. General Abel Kandiho na General Kale Kayihura kwa ukandamizaji wa haki za kibinadamu.

Museveni, ambaye anadai kuwa mlinzi wa sheria na utulivu, hajasema iwapo ana mpango wa kugombea tena urais, wala kuzungumzia shughuli za kisiasa za mwanawe.

Raia wa Uganda wanasemaji kuhusu Muhoozi?

Idadi kubwa ya raia wa Uganda wanatafsiri tabia na vitendo vya Muhoozi Kainerugaba kuwa ushahidi wa kutosha kwamba amepokea baraka za babake kugombea urais wa taifa hilo.

Vyama vya kisiasa vya upinzani vimetangaza kwamba vipo tayari kupambana naye kisiasa.

“Babake Muhoozi amekuwa madarakani kwa mda wa miaka 36, lakini je, vijana wamenufaika?” ameuliza David Lewis Rubongoya, katibu mkuu wa chama cha upinzani cha National Unity Platform -NUP, chake Robert Kyagulanyi, maarufu kama Bobi Wine, akiongezea kwamba idadi kubwa ya watu nchini Uganda ni maskini na hawana ajira.

Bobi Wine alishindwa na Museveni katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2021 licha ya kuwa na ufuasi mkubwa wa vijana, japo kulikuwepo madai ya wizi wa kura. Amemshutumu Museveni kwa kutumia wanajeshi na polisi kuwakandamiza wanasiasa wa upinzani.

"Huwezi kusema kwamba unazingatia sana maslahi ya vijana wakati unawateka nyara na kuwaua," ameongezea Rubongoya.

XS
SM
MD
LG