Wafanyakazi wa uokozi huko Nairobi, Kenya wamemuokoa mtoto wa kike mwenye umri wa mwaka mmoja kutoka kwenye kifusi cha jengo ambalo lilianguka siku ya Ijumaa na kuuwa watu wasiopungua 21.
Shirika la msalaba mwekundu Kenya liliripoti kwamba uokozi wa mapema leo Jumanne, likisema mtoto huyo wa kike amepelekwa kwenye hospitali moja mjini humo akiwa amepungukiwa sana maji mwilini lakini hakuwa na dalili ya majeraha ya kimwili.
Waokozi wamesema kuna matumaini madogo ya kumpata mtu yeyote akiwa hai katika mabaki hayo ya jengo katika kitongoji cha Huruma. Lakini kugunduliwa kwa mtoto huyo kumezusha matumaini kwa wale wanaosubiri kusikia habari kuhusu wapendwa wao ambao bado hawajulikani walipo.
Watu 135 wameokolewa kutoka jengo hilo makazi la gorofa 6 lililoanguka, huku darzeni wakiwa bado hawajulikani walipo, siku tano baada ya kuanguka jengo hilo kufuatia mvua kubwa zinazonyesha nchini humo.