Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 22:28

Mpasuko ndani ya chama cha Republican, Spika hajachaguliwa


Kiongozi wa chama cha Republican katika baraza la wawakilishi Kevin McCarthy (kushoto) wakati wa kuhesabu kura mara ya 4. hakuna msindi alipatikana baara ya kupiga kura mara 6. Januari 4, 2023
Kiongozi wa chama cha Republican katika baraza la wawakilishi Kevin McCarthy (kushoto) wakati wa kuhesabu kura mara ya 4. hakuna msindi alipatikana baara ya kupiga kura mara 6. Januari 4, 2023

Wawakilishi wa chama cha Republican hawajaelewena kuhusu mmoja wao wanayestahili kumuunga mkono na kumchagua kuwa spika wa baraza la wawakilishi.

Kinyang’anyiro ni kati ya wagombea watatu. Mdemokrat Hakeem Jeffries anayewakilisha New York, Mrepublican Kevin McCarthy wa California na Mrepublican mwenzake Andy Biggs wa Arizona.

Warepublican wana idadi kubwa ya wawakilishi katika baraza la Wawakilishi, lakini mgawanyiko unadhihirika baada ya kuwasilisha wagombea wawili kujaza nafasi ya spika na hivyo basi wameshindwa kujaza nafasi hiyo baada ya kura kupigwa mara sita, shughuli ambayo ilianza Jumanne, Januari 3.

Vikao viliahirishwa Jumatano saa mbili usiku saa za Washington DC, na wawakilishi watarejea tena tena kupiga kura mara ya saba.

Hii ni mara ya 15 katika historia ya Marekani, ambapo uchaguzi wa spika haukufanikiwa katika raundi ya kwanza. Mara ya mwisho uchaguzi wa spika ulichukua muda mrefu sana kupata mshindi ilikuwa mwaka 1855, miaka 167 iliyopita. Ilichukua miezi miwili kumpata spika baada ya mivutano kati ya wabunge.

McCarthy ambaye alijondoa kwenye kinyang’anyiro cha spika mwaka 2015 aliposhindwa kuwashawishi wanachama wake wenye mrengo mkali, hajakata tamaa, japo hakuna matumaini ya kumpata spika hadi wakati tunapoandaa ripoti hii.

Namna wawakilishi wamepiga kura mara sita

Mvutano unaendelea ndani ya chama cha Republican, majibizano ya kisiasa yanaendelea huku hali ya sintofahamu ikikaribia.

McCarthy anakumbana na msukumo mkubwa kutoka kwa Warepublican wanaomuunga mkono pamoja na Wademocrat, kutafuta kura za kutosha au ajiondoe kwenye kinyang’anyiro hicho.

Wawakilishi waliochaguliwa katika uchaguzi wa katikati ya muhula hawajaapishwa. Kamati hazijaundwa, wasimamizi wa kamati hawajaapishwa, na hivyo shughuli zote za baraza la Wawakilishi zimekwama.

Warepublican wanaompinga wanaonekana kutolegeza msimamo na wanaendelea kupata wanaowaunga mkono kutoka kwenye kambi ya McCarthy.

Katika duru ya kwanza ya upigaji kura, Mrepublican Biggs anayempinga McCarthy, alipata kura 10, aliongeza kura zake katika duru ya pili na kupata kura 19, kura 20 katika duru ya tatu, ya nne, tano na sita.

McCarthy alipata kura 203 katika duru ya kwanza na ya pili, kura 202 duru ya tatu, 201 duru ya nne, ya tano na sita.

Kura za Mdemokrat Hakeem Jeffries hajizabadilika, 212. Mshindi anastahili kupata kura 218.

kikao cha baraza la wawakilishi la Marekani kumchagua spika January 3, 2023
kikao cha baraza la wawakilishi la Marekani kumchagua spika January 3, 2023

Upigaji kura mara ya 7 au zaidi

Wabunge wanarudi tena Capitol adhuhuri kwa saa za Washington DC kumtafuta atakayewaongoza katika mijadala na shughuli zao. Lakini safari inaonekana kwamba bado ni ndefu, hakuna upande unaonekana kuelegeza msimamo.

Idadi kubwa ya Warepublican huenda wasiwepo bungeni kesho Ijumaa, Januari 6, kumbukumbu ya siku ambayo wafuasi wa aliyekuwa rais Donald Trump walivamia bunge wakipinga ushindi wa Joe Biden.

Mivutano mirefu ndani ya chama cha Republican na kushindwa kumchagua spika kwa haraka bila shaka ni dhihirisho na hali isiyo thabithi ya demokrasia nchini Marekani, baada ya kuvamiwa kwa bunge na wafuasi wa Trump miaka miwili iliyopita.

Spika anayeondoka Nancy Pelosi, mwakilishi wa California, ameandika ujumbe wa Twitter kwamba wabunge wote kwa jumla wana jukumu la kuhakikisha kwamba baraza wa Wawakilishi linaheshimiwa.

Pelosi ameandika kwamba tabia inayoonyeshwa na Warepublican katika uchaguzi wa spika haina heshima na haistahili katika bunge la Marekani na kwamba ni lazima wafungue bunge na kuruhusu shughuli zake kuendelea.

Wanachama wenye mrengo wa siasa za Trump

Andy Biggs, mwanachama wa Republican anayeongoza mrengo wa siasa kali, unaompinga Kevin McCarthy katika kinyang'anyiro cha spika wa bunge la wawakilishi
Andy Biggs, mwanachama wa Republican anayeongoza mrengo wa siasa kali, unaompinga Kevin McCarthy katika kinyang'anyiro cha spika wa bunge la wawakilishi

Warepublican wanaompinga McCarthy ni wanachama wenye siasa kali za mrengo wa Donald Trump, japo Trump alitangaza kumuunga mkono McCarthy.

Mwakilishi wa Colorado, Mrepublican Ken Buck amesema kwamba hawezi kumhimiza McCarthy kujiondoa kwenye kinyang’anyiro hicho na kwamba amemwambia atafute namna ya kupata uungwaji mkono ili achaguliwe kuwa spika.

Wanaomuunga McCarthy hata hivyo wamesisitiza kwamba watampinga hadi mwisho na wananuia kupata kiti cha spika.

Wachambuzi wanasema kwamba hali ya kuchanganyikiwa ndani ya baraza la Wawakilishi la Marekani ni ishara ya hali ngumu kwa Warepublican katika kuendesha bunge ambalo wana idadi kubwa ya wawakilishi ikilinganishwa na Wademokrat.

Endapo hili litatokea, haitakuwa mara ya kwanza kwa Warepublican kuvutana wenyewe kwa wenyewe.

Mwaka 2011, Spika wa 53 Mrepublican John Boehner alikuwa na wakati mgumu kuongoza kundi la Warepublican waliokuwa waasi, na kupelekea shughuli za serikali kufungwa mara kadhaa. Kwa sababu hiyo, alilazimika kustaafu mapema.

Mivutano zaidi ndani ya chama cha Republican

Wachambuzi wa siasa za Marekani wanasema kwamba Warepublican wanaofuata siasa na sera za Donald Trump, za Make America Great Again, wanataka kuzipa umaarufu sera hizo na wanataka kuchukua kila hatua kumzuia McCarthy kuwa spika.

McCarthy anahitaji karibu kura 12 za warepublican kuwa spika.

Ili kupata kura hizo McCarthy anaripotiwa kwamba amekubali matakwa ya Warepublican wenye msimamo huru wanaotaka mabadiliko yatakayowapa ushawishi mkubwa ndani ya chama.

Kundi la kampeni ya McCarthy limetishia kutofadhili kampeni za chama katika majimbo yanayompinga McCarthy.

Baadhi ya Warepublican wamesema kwamba wapo tayari kupiga kura usiku na mchana, wiki baada ya wiki na hata miezi kumzuia McCarthy kuwa spika.

Upinzani kama huu ulionekana mwaka 2015, McCarthy alipolazimika kujiondoa kwenye kinyang’anyiro cha spika baada ya kushindwa kuwashawishi Warepublican wenye siasa za mrengo mkali.

Kulingana na katiba ya Marekani, Spika anashikilia nafasi ya tatu baada ya rais katika utawala wa nchi.

Je, Wademocrat wanaweza kuungwa mkono na Warepublican 6 kupata nafasi ya spika?

Mdemocrat Hakeem Jeffries anayegombea kuwa spika
Mdemocrat Hakeem Jeffries anayegombea kuwa spika

Wademokrat wameendelea kupiga kura ya spika kwa umoja.

Hakeem Jeffries amepata kura zote za Wademokrat 212 katika duru zote saba kufikia sasa.

Iwapo McCarthy atawashawishi Warepublican na kupata kura 213, kura moja zaidi ya mdemocrat, anaweza kuwashawishi Warepublican waliosalia na kutompigia mgombea yeyote kura kando na kusema tu kwamba wapo bungeni na hivyo kuibuka mshindi.

Mbinu hii inakubalika katika kanuni za bunge la Marekani, ambapo mshindi anastahili kuwa tu na idadi kubwa ya kura ilimradi Wawakilishi wengine waseme tu kwamba wapo bungeni wakati wa upigaji kura.

Hii ndio mbinu ambayo Nancy Pelosi na Boehner waliitumia kuchaguliwa kuwa spika waliposhindwa kupata kura 218 za moja kwa moja.

Mwakilishi mmoja wa chama cha Republican, Victoria Spartz wa Indiana, alijitambuslisha tu kwamba yupo bungeni bila ya kupiga kura ya kuunga mkono mgombea yeyote, lakini hilo halikumsaidia McCarthy, badala yake kura zake zilipungua.

XS
SM
MD
LG