Brahim Saadoun, raia wa Morocco aliyezaliwa mwaka 2000, alipewa adhabu ya kifo tarehe 9 Juni yeye na wanaume wawili raia wa Uingereza na mahakama ya jimbo la Donetsk, mashariki mwa Ukraine lililotangaza kujitenga.
Watatu hao walishtumiwa kuwa mamluki wa Ukraine kufuatia uvamizi wa Russia dhidi ya jirani yake.
Amina Bouayach, mwenyekiti wa Baraza la kitaifa la haki za binadamu ( CNDH), aliwasiliana na kamishna mkuu wa haki za binadamu katika serikali ya Russia, chanzo kutoka baraza hilo la haki za binadamu la Morocco kimeiambia AFP Jumapili.
Aliitaka taasisi hiyo ya haki za binadamu ya Russia "kuchukua hatua zinazohitajika kuhakikisha kesi ya haki kwa Brahim Saadoun wakati wa rufaa yake," chanzo hicho kimesema.
Taher Saadoun, baba wa mtuhumiwa, amesema mwanawe, ambaye alipata uraia wa Ukraine mwaka 2020, sio mamluki, akimtaja badala yake "kuwa muathirika wa upotovu".
Lakini Dmytro Khrabstov, rafiki wa Saadoun mwenye umri wa miaka 20, amesema raia huyo wa Morocco alijiunga na jeshi la Ukraine mwaka jana, akiwaambia marifiki zake kwamba anataka kufa kama shujaa.