Wafanya biashara katika soko maarufu la Marikiti mjini Mombasa wamepata hasara kubwa baada ya moto mkubwa kushuhudiwa usiku wa Jumamosi kuamkia Jumapili
Hakuna ripoti za maafa wala majeruhi kufikia sasa huku juhudi za kuzima moto huo zikiendelea.
Magari ya zima moto kutoka kitengo cha serikali za ugatuzi wakishirikiana na polisi wako kwenye tukio wakijaribu kudhibiti hali.
Wakati huu ambapo kuna sharti la kutotoka nje wakati wa usiku kwa sababu ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona, baadhi ya wakaazi wa maeneo ya karibu wako nje kushuhudia moto huo na wengine wakitoa msaada wa kudhibiti moto.
Hali hii imewalazimu maafisa wa kushika doria nyakati hizo kuweka usalama eneo hilo pia kuepusha visa vya uporaji kutokea kwenye baadhi ya maduka yaliyoachwa wazi kutokana na moto huo.
Haijabainika chanzo cha moto huo, na hakuna mwenye kufahamu nini hasa ilikuwa sababu ya moto.