Maafisa kaskazini-magharibi mwa Pakistan wanasema mtu anayeshukiwa kuwa mlipua bomu wa kujitoa mhanga ameuwa watu wasiopungua 41 na kujeruhi wengine kadha. Shambulizi hilo limetokea siku moja baada ya wapiganaji wa Taliban kuanza mashambulizi yaliyofanyika kwa wakati mmoja dhidi ya vikosi vya usalama katika wilaya ya jirani na kuuwa wanajeshi 11.
Bomu hilo la kujitoa mhanga lilitokea katika mji wa Khar, makao makuu ya wilaya ya Bajaur ambayo imekuwa na mashambulizi mengi ya waasi karibu na mpaka wa Afghanistan.
Mashahidi wanasema mlipuko huo mkubwa mara moja uliuwa watu zaidi ya 30 wakati wengine walikufa kutokana na majeraha katika hospitali ya serikali.
Mlipua bomu huyo alilenga eneo lenye watu wengi ambao walikuwa wakipokea misaada katika kituo cha Shirika la Chakula Duniani kilichofunguliwa kusaidia familia zilizopoteza makazi kutokana na mapigano.