Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 20:19

Mkuu wa Jeshi la Pakistani ataka madrasa ziboreshwe


Jenerali Qamara Javed Bajwa
Jenerali Qamara Javed Bajwa

Mkuu wa Jeshi la Pakistan mwenye ushawishi mkubwa ameingilia kati suala nyeti la madrasa za Kiislam akidadisi iwapo shule hizo za dini zinawaandaa wanafunzi katika zama zinazotawaliwa na teknolojia.

Jenerali Qamar Javed Bajwa ameeleza dukuduku lake juu ya madrasa hizo katika semina iliyojikita juu ya maendeleo ya vijana huko Quetta, ambako Marekani na Afghanistan zinafikiria kuwa ndiko chimbuko la kikundi cha Wataliban wa Afghanistan.

Harakati hizo za Wataliban zilianza kati ya wanafunzi waliokuwa wanahudhuria shule za kidini Pakistani.

“Kwa hivyo kitu gani wanaadaliwa kwacho wanafunzi hawa wa madrasa? Je hawa watakuwa mashehe au watakuja kuwa magaidi?” Bajwa amedadisi.

Madrasa hizi huwa zimejikita katika kufundisha usimamizi wa sheria za Kiislam na itikadi za kidini, na zinajiepusha kufundisha zaidi masomo ya hisabati, sayansi na jamii. Kihistoria, wanaomaliza madrasa huwa wanaweza kupata kazi moja : kuwa imam wa msikitini.

Bajwa amesema kuwa ameelezwa kwamba wanafunzi milioni 2.5 wanasoma katika madrasa hizo nchini Pakistani na kuwa ni vigumu kujenga misikiti ambayo itaweza kutosheleza kutoa ajira kwao. Bodi ya Madrasa nchini Pakistani imesajili madrasa takriban 35,337.

Madrasa zimekataa kuitikia wito wa kufanya mabadiliko, zimefeli kukidhi mahitaji ya mifumo ya kisasa ya elimu na nadharia zake na zinatuhumiwa kwa kuzuia wanafunzi kuwa wadadisi na wachambuzi, na wanafunzi wao wanapata shida katika soko la ajira kwani hawawezi kushindana katika uchumi unaotaka mtu awe na taaluma maalum.

“Inatulazimu tuangalie upya na kuzifanyia tathmini tena nadharia za madrasa hizi,” Bajwa amesema.

“Nyingi katika madrasa hizi zinafundisha dini peke yake. Kwa hivyo vipi wana wawezesha wanafunzi wao kupata ajira? Nini mustakbali wao katika nchi hii? Inatulazimu tuwape taaluma inayoendana na mifumo ya dunia ya leo.”

Qibla Ayaz, mkuu wa Baraza la Falsafa za Kiislam, Waangalizi wa masuala ya dini Pakistani, ameiambia VOA kuwa mjadala kuhusu mabadiliko ya madrasa hizi ni lazima yashirikishe mfumo mzima wa elimu nchini Pakistani.

“Ukiangalia wanafunzi kutoka katika shule za kisekula, wengi wao pia hawapati ajira,” amesema Ayaz.

“Elimu yetu haiwapi ujuzi wanafunzi wetu, na hivyo basi tunashuhudia vitendo vya kigaidi, vikifanywa na wanafunzi kutoka Chuo Kikuu cha Karachi, Chuo Kikuu cha Lahore na vyuo vingine maarufu wanafunzi wao wakishiriki katika ugaidi.

Mjadala kuhusu maboresho katika madrasa hizi siyo jambo geni, lakini hivi sasa limekuwa na umuhimu kutoka na kuongezeka vitendo vya uvunjifu wa amani, ambapo lawama nyingi za uvunjifu huo wa amani zinaelekezwa kwa wanafunzi wa madrasa na viongozi wao, ambao wakosoaji wa madrasa hizo wanadai kuwa zinashawishi uvunjifu wa amani, kutovumiliana na chuki dhidi ya nchi za Magharibi.

XS
SM
MD
LG