Trump katika ziara yake ya kwanza nje ya nchi akiwa Rais, amesema kuwa Marekani inataka kuwepo mseto wa nchi “unaoshirikiana katika lengo la kutokomeza siasa kali,” akieleza vita hivyo kuwa ni “mapambano kati ya mema na maovu.”
“Hii sio vita kati ya imani mbalimbali za kidini, madhehebu mbalimbali, au tamaduni mbalimbali,” Trump amesema katika baadhi sehemu ya hotuba yake iliyotolewa na ikulu ya White House.
“Hii ni vita kati ya watu wenye kufanya ujangili wa kinyama ambao wanataka kuangamiza uhai wa wanadamu na upande wa wale ambao ni watu wastaarabu wa dini zote ambao wanataka kulinda uhai wa binadamu.”
Trump ambaye anataka kuzuia Waislam kutoka katika nchi sita zenye Waislam wengi zaidi ambako vitendo vya ugaidi vimewahi kutokea kuingia Marekani, hakutumia tamko la “ugaidi wa Kiislam wenye siasa kali” katika hotuba yake, kama ilivyokuwa akifanya hivyo mara nyingi katika hotuba zake nchini Marekani.
Badala yake, amewataka viongozi wa Kiislam kuwa wakweli katika kupambana “na mgogoro wa vikundi vya Kiislam venye misimamo mikali na vikundi vya kigaidi vya Kiislam ambavyo magaidi hao wanavihamasisha.”
Amesema kuwa, “Marekani ni nchi huru na kipaumbele chetu cha kwanza siku zote ni usalama na amani ya raia zetu. Hatukuja hapa kuwafundisha – hatuko hapa kuwaambia watu jinsi ya kuishi, nini wafanye, wawe namna gani, au jinsi ya kuabudu.
Lakini tuko hapa kutoa ushirikiano—kwa yale yenye misingi na maslahi kwa pande zote – ilikujenga mustakbali bora kwa kila mmoja wetu. Kila wakati gaidi anapoua mtu asiyekuwa na hatia na kusingizia amefanya kwa ajili ya Mungu, iwe ni tusi kwa kila mtu mwenye imani yake.”
“Ugaidi umeenea ulimwenguni,” amesema Trump. “Lakini njia ya amani inaanzia hapa tulipo, katika asili hii ya kihistoria, katika ardhi hii takatifu,” akisisitiza kuwa “Marekani iko tayari kusimama mstari mmoja na nyinyi—katika kuhakikisha maslahi yetu ya pamoja na usalama wetu wa jumla.”