Kremlin inaangaza lengo moja muhimu: Ni kuirudishia Russia hadhi yake muhimu katika uwanja wa kimataifa baada ya kutengwa na kutaka kurejea kuwa msuluhishi wa masuala ya mvutano ulimwenguni.
Kabla ya mkutano huo, Rais Trump – baada ya wiki ya utata akifanya mikutano na washirika wa Marekani wa muda mrefu huko Brussels na London amesema kuwa mazungumzo yake na kiongozi wa Russia “yatakuwa pengine ni mepesi kuliko mikutano yote aliofanya.”
Hata hivyo, wachambuzi wa masuala ya Russia wametahadharisha kuwa Trump atakabiliwa na mzungumzaji mjanja ambaye mjadala wake – umeboreshwa vizuri kutokana na uzoefu wa kuwa ameshikilia madaraka kwa miaka 18.
“Kwa Putin, siku zote kuna njia ya kurudia kile ambacho siku zote amekisema : ‘Russia haijawahi kufanya kitu chochote kibaya. Russia haina haja ya kuboresha wala kubadilisha kitu chochote,” amesema Maria Lipman, mhariri wa jarida la Counterpoint huko Moscow, linalo chapishwa na Taasisi inayoshughulikia tafiti za Ulaya, Russia na Eurasian katika Chuo Kikuu cha George Washington, Marekani.
"Iwapo Marekani inataka kubadilisha sera zake, tunawakaribisha. Sisi hatuna kitu cha kujutia, hakuna cha kusahihisha,” ameongeza, akieleza msimamo wa Kremlin katika miaka ya hivi karibuni.