Rais mteule, Donald Trump anatarajiwa leo Jumatano kufanya kikao na wanahabari baada ya karibu miezi 6 ikitarajiwa kuwa atakumbana na maswali kadhaa na hasa kuhusu madai kutoka kwa idara za upelelezi za Marekani kuwa Russia iliingilia uchaguzi alioshinda mwezi Novemba, na jinsi atakavyotenganisha bishara zake binafsi na kazi za urais.
Mara ya mwisho Trump kufanya kikao na wanahabari ilikuwa mwezi Julai ambapo alimshambulia mpinzani wake wa kutoka chama cha Demokratik, Hillary Clinton kwamba alichukua miezi kabla ya kuzungumza na wanahabari.
Marais wengi wa Marekani hutoa hotuba kwa wanahabari muda mfupi baada ya kuchaguliwa kinyume na Trump ambaye amekuwa akitumia akaunti yake ya Twitter na ujumbe mfupi lakini hajakutana rasmi na kundi la wanahabari kujibu maswali.