Wajumbe wa Republican nchini Marekani wanaanza kukutana wiki hii huko Charlotte kwenye jimbo la North Carolina, ambapo wanatarajiwa kumteuwa Rais Donald Trump kama mgombea wao atakayekabiliana na M-democrat Joe Biden, Makamu Rais wa zamani kwenye kinyang’anyiro cha uchaguzi mkuu wa urais mwezi Novemba.
Rais Trump anakabiliana hivi sasa na matatizo ya uchumi, maandamano yanayoendelea juu ya dhuluma za kijamii na rangi, Pamoja na kukosolewa kufuatia namna alivyoshughulikia janga la virusi vya Corona ambalo limeuwa zaidi ya wamarekani 176,000 huku akiwa nyuma ya Biden kwenye kura nyingi za maoni ya kitaifa. Hata hivyo mkuu wa wafanyakazi wa White House, Mark Meadow amesifia maadili ya kazi za mkubwa wake huku akitilia mkazo anastahili kuendelea na muhula wa pili.
"Rais kila siku, sio tu amejiandaa, lakini anafanya kazi kubwa kuliko rais yeyote ambaye nimewahi kupata fursa ya kumfanyia uchunguzi na kusoma kuhusu kile anachotaka kuhakikisha kwamba tunasonga mbele katika wakati mgumu, ajenda muhimu kwa watu wa kawaida Marekani wanaofanya kazi kwa bidii".
Wakati huo huo mpinzani wa Rais Trump, Joe Biden aliweka historia wiki iliyopita kwa kumteuwa seneta Kamala Harris, kama mgombea mwenza wake. Harris ni mwanamke wa kwanza mweusi kuteuliwa kwenye wadhifa huo na chama kikubwa cha kisiasa, na naibu meneja kampeni, Kate Beningfield, anasema lengo la Biden ni ushirikishwaji na ahadi ya kuponya taifa wakati linakabiliwa na janga la virusi vya Corona.
"Kama Rais, Joe Biden ataweza kuwakutanisha watu kwenye meza moja, kukamilisha changamoto muhimu na kupata nafuu kwa watu ambao wanahitaji hilo, kwenda kwa wafanyabiashara wadogo ambao wanaumia hadi familia zinazofanya kazi ambazo zinaumia".
Takribani wajumbe wa Republican 336, kati ya zaidi ya 2,400 watakuwa Charlotte, Jumatatu baada ya hapo mkutano wa chama hicho utahamia kwenye maeneo yanayofanya matukio kwa njia ya video.
Wanafamilia wengine wa Rais Trump watazungumza kwenye matukio mbali mbali wiki hii, akiwemo mkewe Melania Trump. Rais anatarajiwa kuonekana kila siku usiku kuanzia Jumatatu, na siku ya Alhamis atatoa hotuba akiwa White House ya kukubali rasmi uteuzi wa chama kuwania muhula wa pili madarakani.