Biden alitua katika uwanja wa ndege katika mji mkuu wa Namibia Windhoek Jumatano alasiri kabla ya kuelekea Heroes' acre, eneo la kumbukumbu ya vita, pamoja na mke wa rais wa Namibia.
Safari yake itaangazia elimu, afya na kuwawezesha vijana na wanawake, alisema katika taarifa yake kwenye mitandao ya kijamii. Baada ya Namibia atakwenda nchini Kenya ambako atasikia kutoka kwa wale walioathiriwa na ukame na uhaba wa chakula, alisema.
Utawala wa Biden unapanga kufanya ziara kadhaa za ngazi ya juu barani Afrika mwaka huu katika juhudi za kukabiliana na ushawishi wa China na Russia katika bara hilo.
Kwa sasa Afrika Kusini ni mwenyeji wa mazoezi ya pamoja ya jeshi la majini kati ya Russia na China, hatua ambayo nchi hiyo inasema ni ya kawaida lakini imeitia wasiwasi Marekani na washirika wengine wa Magharibi.
Ni safari ya kwanza ya Jill Biden barani Afrika kama mke wa rais.