Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatano, Januari 22, 2025 Local time: 23:44

Wachambuzi wasema mkataba wa bandari kati ya Tanzania na Dubai una utata


Rais Tanzania Samia Suluhu akiwa Dodoma tarehe 22 Aprili , 2021.
Rais Tanzania Samia Suluhu akiwa Dodoma tarehe 22 Aprili , 2021.

Wachambuzi wa masuala ya uchumi na wanasheria wameukosoa mkataba wa ushirikiano wa kiuchumi na kijamii kati ya serikali Tanzania na Dubai, na kusema kuwa mkataba huo hauna uwazi na kuitaka serikali Tanzania kutoa ufafanuzi wa baadhi ya vifungu venye utata.

Wachumi na wanasheria wameeleza kutoridhishwa na baadhi ya ibara zilizopo ndani ya mkataba huo wenye lengo la kuimarisha usimamizi na utendaji kazi kwenye bandari kuu ya Dar es Salaam.

Miongoni mwa ibara hizo ni ile ya 23 ambayo inaeleza kuwa serikali husika katika mkataba huo hazitakuwa na haki ya kuvunja mkataba, kujitoa, kuahirisha au kusitisha mkataba katika mazingira yoyote.

Joseph Oleshangay wakili kutoka Arusha amesema mkataba huo unaweza kuleta athari kubwa kitaifa iwapo utavunjwa siku za usoni.

“Kwasababu huu mkataba ukiuvunja leo ama baada ya miaka miwili tutakacho lipa itakuwa na madhara makubwa kwa uchumi wa nchi yetu.” Na aliongeza “Lakini tunahitaji pia kuangalia madhara ya kuendelea nayo ama madhara ya kuvunja yapi yatakuwa na madhara madogo, twende na hizo njia ambazo zitakuwa na manufaa kiasi kwa nchi yetu” alisema Oleshangay.

Hatua hiyo ya kuwapa wadau nafasi ya kutoa maoni umefanyika wiki chache baada ya ripoti ya utafiti ya Benki ya Dunia kutoa toleo lake la tatu la Container Port Performance Index 2022, inayosema kwamba Bandari ya Dar es Salaam inashika nafasi ya 312 duniani ikiiongoza bandari ya Mombasa ambayo imeshika nafasi ya 326.

Aidha, wachumi wamesema mkataba huo utaiondoa Tanzania katika kujenga uchumi endelevu kutokana na kasoro nyingi, na kutaifanya Tanzania kukosa uhuru wa kiuchumi kwa kuwa kampuni ya Dubai DP World imekuwa na changamoto katika mataifa mengine yaliyowekeza wekeza na kampuni hiyo.

Mchumi na mhadhiri wa chuo kikuu cha kimataifa cha Kampala tawi la Dar es Salaam Dr.Bravious Kahyoza amesema. “Na nimuhimu tukakumbuka kwamba bandari ya Dar es Salaam ni moja ya viungo vikuu vya uchumi wetu unapo uondoa mikononi mwa serikali unasababisha vitu vikubwa viwili kwenye uchumi moja ni kukosekana kwa uhuru wa nchi kumbuka kampuni hii imekuwa na makandokando yanamna hiyo kwenye nchi nyingi.”

Mbali na wachumi na wanasheria suala hili limewaibua wanasiasa wa upinzani ambao pia wameonyesha kutoridhishwa na baadhi ya ibara zilizomo katika mkataba huo, miongoni mwao ni Mwenyekiti wa Taifa chama cha Demkrasia na Maendeleo CHADEMA Freeman Mbowe ambaye ana mashaka kuhusu bandari ya Zanzizar ambayo haimo katika katika mkataba huo.

“Swali la wazi hapa ni je, kama kweli mkataba huu unamanufaa makubwa kwa nchi zetu kama inavyodaiwa na serikali ya ccm kwanini bandari za Zanzibar hazimo kwenye mkataba huu.” Alisema Mbowe.

“kwasababu kama bandari ni jambo la muungano jambo hili ili liondowe hizo hisia ambazo ni hasi na zinajengwa miongoni mwa Watanzania na hususani wa Tanganyika,” aliongeza Mbowe.

Hata hivyo katika vikao vya bunge vinavyoendelea huko Dodoma spika wa bunge la Tanzania Dkt. Tulia Ackson amesema mchakato wa kupokea maoni bado unaendelea mpaka tarehe 10 mwezi Juni, ambako mkataba huo utapelekwa bungeni.

Ripoti hii imetayarishwa na Amri Ramadhani, Sauti ya Amerika, Dar es Salaam

Forum

XS
SM
MD
LG