Kwa mujibu wa shirika la habari la AFP, mjadala huo wa kitaifa unaohusisha makundi mbali mbali kwa lengo la kurejesha utawala wa kiraia ulianza mwezi uliopita, ukipangwa kumalizika Septemba 20. Tarehe ya mwisho sasa imesogezwa hadi Septemba 30. Mazungumzo hayo yameahirishwa mara kadhaa hapo mbeleni baada ya makundi yenye silaha pamoja na makundi ya upinzani kususia, yakidai kwamba mazungumzo hayo ni kati ya serikali na washirika wake wa karibu.
Rais wa Chad Mahamat Idriss Deby Itno anaongoza baraza la kijeshi lenye wajumbe 15, baada ya kuchukua madaraka, kufuatia kifo cha baba yake wakati akiwa kwenye uwanja wa vita dhidi ya waasi Aprili 2021. Kiongozi huyo amebuni mjadala wa kitaifa kwa nia ya kuitisha uchaguzi huru na wa kidemokrasia katika kipindi cha miezi 18. Kikao hicho hicho kufikia sasa hakijapiga hatua kubwa kuelekea kwenye malengo yake.