Kwa mujibu wa shirika la habari la Reuters, wizara hiyo katika taarifa imesema kwamba mlipuko huo sasa umesambaa kote nchini na kusababisha asilimia 6.9 ya vifo miongoni mwa walioambukizwa. Waziri wa Afya Jasper Chimedza amesema kwamba kufikia Alhamisi wiki iliyopita, kulikuwa na kesi 1,036 zilizoshukiwa kuwa za surua, wakati 125 zikithibitishwa tangu kutokea kwa mlipuko huo.
Jimbo la Manicaland mashariki mwa Zimbabwe linasemekana kuongoza kwa maambukizi. Chimedza ameongeza kusema kwamba kesi ya kwanza iliripotiwa Aprili 10 na tangu wakati huo maambukizi yameenea kote nchini, yakisemekena kuchochewa zaidi na mikusanyiko ya waumini makanisani.
Wengi walioambukizwa ni watoto wenye umri kati ya miezi 6 na 15, wengi wakitokea kwenye familia za waumini waliokataa chanjo dhidi ya surua kutokana na imani za kidini. Baadhi ya madhehebu nchini Zimbabwe huwakataza wafuasi wao kupokea aina yoyote ile ya chanjo au matibabu. Madhehebu hayo yana mamilioni ya wafuasi wanaoamini miujiza ya uponyaji pamoja na kujikwamua kutoka kwenye umaskini.