Mshambuliaji wa kujitoa muhanga aliendesha gari hilo lililokuwa limesheheni vilipuzi akilielekeza kwenye kituo cha ukaguzi wa usalama katika mji wa Beledweyne siku ya Jumamosi, na kusababisha mlipuko ambao ulipelekea watu wengi kukwama chini ya matofali.
Polisi wameliambia shirika la habari la AFP leo Jumapili kwamba idadi ya waliofariki imeongezeka na kuvuka vifo 13 vilivyoripotiwa awali lakini hawakutoa idadi kamili.
“Operesheni ya kutafuta na kusafisha imeendelea kwenye eneo la mlipuko na maiti zilipatikana Jumapili asubuhi chini ya vifusi vya baadhi ya majengo,” amesema Sayid Ali, naibu kamanda wa kituo cha polisi cha Beledweyne.
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud alilaani shambulio hilo, lakini alionekana kubadili kauli juu ya azma yake ya “kuwatokomeza” wanamgambo wa Al-Shabab ambao wameendesha uasi dhidi ya serikali kuu tete ya nchi hiyo kwa zaidi ya miaka 15.
Alisema “ Matukio kama haya hayatatuvunja moyo kamwe kwa kuendelea na harakati za kuwatokomeza magaidi.”
Hakuna kundi lililodai kuhusika na shambulio la Jumamosi.
Forum