Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumanne, Desemba 24, 2024 Local time: 19:12

Michael Cohen akiri kuvunja sheria za kampeni ya uchaguzi Marekani


Aliyekuwa wakili na rafiki wa karibu wa rais Dionald Trump, Michael Cohen, anaonekana hapa akiondoka kwenye jengo la mahakama moja ya Manhattan mjini New York siku ya Jumanne baada ya kukiri kuvunja sheria mbalimbali.
Aliyekuwa wakili na rafiki wa karibu wa rais Dionald Trump, Michael Cohen, anaonekana hapa akiondoka kwenye jengo la mahakama moja ya Manhattan mjini New York siku ya Jumanne baada ya kukiri kuvunja sheria mbalimbali.

Baada ya vuta nikuvute kati ya waendesha mashtaka na mawakili wa aliyekuwa wakili na mshauri wa karibu wa Rais Donald Trump, hatimaye Michael Cohen Jumanne alikiri kuvunja sheria nane zikiwa ni pamoja na ubadhirifu wa fedha za kampeni na kuwalipa wanawake wnawake "waloshiriki ngono na mteja wangu."

Cohen alisema kwamba aliwalipa wanawake hao ili kuwanyamazisha wasitoe habari zozote kuhusu uhusiano wa kingono ambao, alisema, walikuwa nao na rais Trump kabla ya mteja wake, ambaye wakati huo alikuwa mfanyabiashara maarufu, kujitosa uwanjani kuwania urais.

Mwanasheria huyo alikiri kwamba alifanya udanganyifu na kutoa habari za uongo kwa benki.

Hali kadhalika alikiri kutoa michango mikubwa ya kampeni kinyume cha sheria na baadaye kudai malipo kwa njia ya udanganyifu.

Aidha rafiki huyo wa zamani wa Rais Trump alikiri kwamba alitekeleza uhalifu huo kwa niaba ya mgomea wa uchaguzi ambaye alimwelekeza kufanya hivyo. Waendesha mashtaka wamekuwa wakisisitiza kwamba mgombea huyo alikuwa ni rais wa sasa wa Marekani, Donald Trump.

Cohen alimwambia jaji wa mahakama moja ya Manhattan, mjini New York, kwamba kimsingi malipo hayo yalikuwa yanakusudiwa kuisaidia kampeni ya urais ya mwaka wa 2016.

Aidha, Cohen alikiri kuvunja sheria za kanuni za kuweka pesa kwenye benki na ulipaji kodi kwa kutotoa habari za kweli kuhusu hali yake ya kifedha.

Kwa muda mrefu Cohen alifahamika kama rafiki mkubwa wa Trump na kuhudumu kama wakili wake kwa zaidi ya mwongo mmoja.

Wakili huyo aliwahi kusema kwamba angejitolea kupigwa risasi kwa niaba yake.

Kukiri kwa Cohen kumejiri baada ya miezi kadhaa ya uchunguzi ulioangaziwa sana na vyombo vya habari vya Marekani.

Cohen huenda akapata kifungo cha miaka sita kwa makosa hayo.

Wakili wake alitoa taarifa fupi iliyosema kuwa "mteja wangu ameamua kushirikiana na waendesha mashtaka ili kuharakisha mchakato huu na ili maisha yake na ya familia yake yasonge mbele."

Mwezi Mei, Cohen aliwashangaza wengi alipoonekana kujitenga na rais Trump kwa kusema wakati wa mahojiano na kituo kimoja cha televisheni kwamba kipau mbele chake ni familia na nchi yake.

Jumanne, wakili wa binafsi wa Rais Trump, Rudy Guiliani aliandika ujumbe kupitia mtandao wa Twitter uliosema kwamba Cohen alifanya uhalifu kwa niaba ya watu wengine lakini mteja wake (Trump) hakuhusika kwa vyovyote.

Kwingineko, aliyekuwa mwenyekiti wa kampeni ya Donald Trump, Paul Manafort, mapema Jumanne alipatwa na hatia ya makosa 8 kati ya mashtaka 18 yaliyokuwa yakimkabili.

Kesi ya Manfort ilikiuwa inasikilizwa katika mahakama moja mjini Alexandria, jimbo la Virginia.

Aliyekuwa mwenyekiti wa kampeni ya Donald Trump. Paul Manafort. Juni 15, 2018.
Aliyekuwa mwenyekiti wa kampeni ya Donald Trump. Paul Manafort. Juni 15, 2018.

Manafort, ambaye pia alikuwa anashutumiwa kwa ubadhirifu wa fedha aliposimamia kampeni ya urais ya mwaka wa 2016 kama mwenyekiti, huenda akapata kifungo cha zaidi ya miaka 50 kwa kupatikana na hatia.

Na akizungumza na waandishi wa habari Jumanne jioni, rais Trump alisema alikuwa amesikitishwa mno na habari kuhusu kupatikana na hatia kwa Manafort na kusema kwamba alikuwa "mtu mwema ambaye anadhulumiwa bure."

Hata hivyo, alipoulizwa kutoa kauli kumhusu Cohen, Rais Trump hakusema lolote, na badala yake akaingia kwenye gari lake na kuondoka.

XS
SM
MD
LG