Mmoja wa wafanyakazi wawili wa shirika la ndege ya Kenya waliokamatwa katika nchi jirani ya Jamhuri ya Kidemokrasi ya Congo mwezi uliopita ameachiliwa, maafisa waandamizi wa Kenya wamesema siku ya Jumatatu.
Kukamatwa kwa wafanyakazi hao wawili wa Kenya Airways kulilifanya shirika hilo April 29 kusimamisha safari za ndege kwenda mji mkuu Kinshasa siku iliyofuata.
Tunashukuru sana kuwajulisha kuwa Lydia Mbotela, meneja wa shirika hilo nchini DRC ameachiliwa hivi punde na mamlaka huko Kinshasa, Korir Sing”oe katibu mkuu wa wizara ya mambo ya nje ameandika kwenye mtandao wa X ambao zamani ulijulikana kama Twitter.
Hakutoa maelezo zaidi kuhusu hatima ya mwenzake wa pili ambaye bado anashikiliwa na hakuna maoni yeyote kutoka shirika la Kenya Airways.
Wafanyakazi hao wawili ambao walikuwa wanafanya kazi kwenye ofisi ya shirika hilo mjini Kinshasa, walikamatwa April 29 na kitengo cha kijasusi cha kijeshi kwa mujibu wa Kenya Airways.
Shirika hilo limeeleza kuwa kukamatwa kwao ni kinyume cha sheria na kunalenga kuinyanyasa biashara ya Kenya Airways.
Tukio hilo limechochea ghadhabu nchini Kenya huku kamati yenye nguvu ya bunge ikisema ni ukiukaji wa kanuni za kidiplomasia.
Forum