Hii itakuwa mara ya kwanza kwa Bi Trump kuzuru bara hilo.
Katika taarifa iliyotolewa na afisi ya Bi Trump, mke huyo wa rais anatazamia kujifunza kuhusu changamoto zinazowakabili watoto wa bara hilo.
“Ni wazo la kusisimua kwamba nitazuru Afrika na kujifunza kuhusu masuala ya watoto tamaduni na historia za bara hilo.”
Rais Donald Trump hajazuru bara hilo tangu aingie madarakani na ameshutumiwa kwamba alitoa maneno ya matusi mapema mwaka huu, yaliyoelekezwa kwa nchi za bara hilo.
Melania Trump hata hivyo amesema kwamba anaamini utengamano duniani ni muhimu na kwamba mazungumzo kati ya jamii mbalimbali yana manufaa makubwa kwani “yanachangia katika mchakato wa kujifunza kutoka kwa jamii mbalimbali.”
Msemaji wa Bi Trump, Stephanie Grisham, amesema kwamba White House itatoa ratiba rasmi na orodha ya nchi atakazotembelea katika wiki chache zijazo.