Kuwekwa kizuizini kwa Andrew Brunson kwa miaka miwili, mchungaji wa kanisa la kiinjili kutoka mji wa Black Mountain, jimbo la North Carolina, zimeyumbisha mahusiano kati ya Uturuki na Marekani, wote wakiwa ni washirika wa Umoja wa kujihami wa NATO.
Ripoti za kuhamishwa mchungaji huyo zimetolewa wiki moja baada ya mahakama ndani ya eneo la gereza upande wa magharibi mwa Uturuki katika mji wa Alaga ilitoa uamuzi kuwa Brunson aendelee kuwekwa kizuizini wakati kesi yake inaendelea.
Mahakama hiyo pia ilitupilia mbali ombi la wakili wa Brunson kuwa aachiwe huru wakati akisubiri maamuzi ya kesi hiyo, ambayo ili ahirishwa hadi Octoba 12. Haijajulikana ni lini Brunson atahamishwa.
Brunson ana kesi ya kujibu kwa tuhuma za kusaidia mtandao ambao Uturuki inaulaumu kwa jaribio la kupindua serikali ya Rais Recep Tayyip Erdogan 2016, pamoja na kuhusika na kuwasaidia wapiganaji wa Kikurdi ambao wamepigwa marufuku kisheria.
Mchungaji huyo mwenye umri wa miaka 50, ambaye anakanusha tuhuma hizo, anaweza kukabiliwa na kifungo cha hadi miaka 35 jela iwapo atapatikana na makosa.
Rais Donald Trump wa Marekani mara kadhaa ameitaka Uturuki kumuachia Brunson.
Wiki iliopita Trump alituma ujumbe wa tweet akisema Brunson kuwekwa kizuizini ni “udhalilishaji kamili” na kuongeza kuwa, “Hajafanya kosa lolote, na familia yake inamhitaji!’