Rais wa Kenya Uhuru Kenyatta amesaini mswaada wa marekebisho ya sheria za tume ya uchaguzi nchini humo IEBC, na kuwa sheria, ili kufanikisha kuundwa kwa jopo la watu saba litakaloteua makamishna wapya wa tume hiyo kuunda nafasi za makamishna wanne waliojiuzulu baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Hatua ya kuteua makamishna hao inaendelea kuibua hisia chungu nzima nchini humo kutoka kwa wanasiasa.
Sheria hiyo mpya, inaifanyia marekebisho sheria namba 9 ya mwaka 2011 ya tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC na inatoa mwongozo wa kubuni jopo litakalokuwa na jukumu la kutangaza, kuhoji na kufanikisha mchakato wa kuajiri makamishna wa uchaguzi ambao mwishowe watateuliwa na rais.
Hatua ya sheria hiyo kufanyiwa marekebisho inatoa udhaifu uliokuwepo kwenye sheria za uchaguzi nchini Kenya, ambapo hapakuwa na utaratibu wa kupata makamishna wapya iwapo waliopo wangejiuzulu kabla au baada ya uchaguzi.
Rais Uhuru Kenyatta anatarajiwa sasa kubuni jopo hilo la watu saba kutoka kwa tume ya utumishi wa umma, tume ya huduma za bunge, tume ya maadhili na kupambana na ufisadi EACC, baraza la mawakili nchini Kenya LSK, miongoni mwa taasisi nyingine.
Tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC, imekuwa ikiendesha shughuli zake kwa takriban miaka miwili ikiwa na makamishna watatu pekee.
Makamishna hao ni Wafula Chebukati ambaye ni mwenyekiti, Boya Molu na Abdi Guliye.
Sheria ya Kenya inasema kwamba lazima tume hiyo iwe na makamishna saba.
Makamishna Roselyn Akombe, Connie Nkatha, Paul Kibiwott Kurgat na Margaret Mwachanya, walijiuzulu miaka miwili iliyopita kwa kile walidai kama kuingiliwa kwa kazi ya tume hiyo na watu kutoka nje ya tume.
Katibu na afisa mtendaji wa IEBC Ezra Chiloba alifutwa kazi mwezi Oktoba mwaka 2018 kwa tuhuma za matumizi mabaya ya pesa za tume hiyo wakati wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2017.
Naibu rais William Ruto ameeleza wasiwasi kuhusu wanasiasa kuhusika katika uteuzi wa makamishna wa IEBC.
“Watu wengi wanasumbuka na wanatuambia kwamba wanataka kuchagua makamishna wapya wa IEBC. Sisi hatuna shida na IEBC. Wachaguliwe wale wanachaguliwa kwa IEBC. Sisi tunajua kura inaamuliwa na wananchi.” Amesema William Ruto.
Rasimu ya jopo la maridhiano maarufu BBI, inalenga kuifanyia mabadiliko katiba ya Kenya.
Rasimu hiyo inapendekeza kuundwa kwa tume mpya ya uchaguzi IEBC kusimamia uchaguzi mkuu wa mwaka 2022.
Imetayarishwa na Mwandishi wetu wa Nairobi Kennedy Wandera.