Mawaziri wa Fedha nchi za Afrika wameeleza kuridhika kwao kutokana na mageuzi yaliyotangazwa na Benki kuu ya Dunia na Shirika la Fedha Duniani yanayopatia mataifa ya Afrika sauti katika baraza la utawala la taasisi hizo za fedha duniani.
Akizungumza kwa niaba ya mawaziri wa fedha wa Afrika waziri wa fedha wa Kenya Uhuru Kenyatta amesema mawaziri wamepongeza mageuzi hayo lakini amesema kunahitajika mazungumzo zaidi kuhakikisha Afrika inanafasi kubwa zaidi katika taasisi hizo kutokana na idadi ya mataifa na ukuwaji wa uchumi unaotokea katika bara hilo.
Katika mutano na waandishi habari mawaziri wa Afrika walisisitiza pia juu ya haja ya kuimarisha miundo mbinu kati ya nchi zao ili kuweza kuimarisha biashara na kutafuta njia mpya za ushirikiano ambao hautategemea misaada ya kigeni pekee yake.
Kenyatta alisema wakuu wa kanda mbali mbali za Afrika wamechukua hatua kuimarisha miundo mbinu kati ya nchi zao ili kuweza kuimarisha biashara. Hata hivyo alizsisitiza kwamba uwezo kamili wa Afrika unaweza kuimarishwa kutokana na uwekezaji wa kigeni. Alisema "Kupanga ajenda ya kuvutia wawekezaji na kubuni nafasi za ajira zinaweza kua sehemu ya mpango wa kufufua uchumi wa dunia."