Upatikanaji viungo

Breaking News
Ijumaa, Novemba 22, 2024 Local time: 17:32

Mawakili wa William Ruto na tume ya uchaguzi wamesisitiza kwamba uchaguzi ulifuata sheria


Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya IEBC Wafula Chebukati (kushoto) akimpokeza cheti cha ushindi kwa rais mteule Dr. Willia Ruto (kulia) Agosti 15 2022. Ushindi wa Ruto umepigwa mahakamani. Picha: Reuters
Mwenyekiti wa tume ya uchaguzi Kenya IEBC Wafula Chebukati (kushoto) akimpokeza cheti cha ushindi kwa rais mteule Dr. Willia Ruto (kulia) Agosti 15 2022. Ushindi wa Ruto umepigwa mahakamani. Picha: Reuters

Tume ya uchaguzi nchini Kenya IEBC imeambia mahakama ya juu kwamba ilifanya kura ya urais kwa kufuata sheria, na kukariri kwamba makosa madogo yaliyosababishwa na tume katika kujumlisha na kuthibitisha matokeo ya kura hiyo hayatoshi kubatilisha matokeo ya kura ya urais.

Rais mteule Dr. William Ruto kupitia kwa mawakili wake, ameiambia mahakama hiyo ya majaji saba kuwa alichaguliwa kihalali na iwapo mahakama itakubali maombi ya Raila Odinga na kubatilisha ushindi wake, basi nchi itaingia kwenye mgogoro wa kikatiba kwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta bado yuko kwenye ofisi lakini amefungwa mikono kikatiba na hawezi hata kumteua mtu yeyote ofisini.

Jopo la majaji 7 wakiongozwa na Jaji Mkuu Martha Karambu Koome, mawakili wa tume ya uchaguzi Prof Githu Muigai, Eric Gumbo, Mahat Somane, na Kamau Karori wameithibitishia mahakama kuwa IEBC kuwa ilifanya kura ya urais kwa kufuata sheria, na miongozo yote inayohitajika katika ufanyikaji wa kura hiyo kwa mujibu wa Kifungu cha 138 (3) (c) na 138 (10) cha katiba ya Kenya.

Amekariri kwamba makosa madogo madogo yaliyojitokeza katika kujumlisha na kuthibitisha matokeo hayo ya kura ya urais hayatoshi kubatilisha ushindi wa Dr. William Ruto.

Wakili wa IEBC wamesisitiza kwamba mwenyekiti anajua vyema sheria

Professa Githu Muigai, ameeleza kuwa Wafula Chebukati, kwa kuwa wakili anafahamu athari ya kukiukwa kwa sheria na kiapo cha majukumu alichochukua na kusisitiza kuwa kinachofanyika sasa ni muendelezo wa nia mbovu dhidi ya tume ya uchaguzi.

Aidha, Muigai anaeleza kuwa ushahidi uliowasilishwa ni porojo tupu na mahakama haiwezi kutegemea porojo kubatilisha kura hiyo.

Na iwapo teknolojia iliyotumiwa na IEBC ilikidhi viwango vya uadilifu, uthibitisho, usalama na uwazi ili kuhakikisha matokeo sahihi na yanayoweza kuthibitishwa, na iwapo kulikuwa na uingiliaji wa upakiaji na uwasilishaji wa Fomu 34A kutoka vituo vya kupigia kura hadi seva ya IEBC, tume hiyo kupitia wakili Eric Gumbo anasema kuwa fomu 34A ina vipengele nane vya usalama,na ngome mbili thabiti na zinazozuia udukuzi wa aina yoyote.

Namna matokeo yalivyonakiliwa kidijitali

Wakili Gumbo ameeleza kuwa baada ya fomu 34A kujazwa, nakala yake hupakiwa kwenye seva ya IEBC na nyingine halisi hupelekwa kwenye kituo cha kuhesabia kura za eneo bunge ambako maajenti wa vyama huwa na haiwezekani kughushi fomu hizo.

Ruto asisitiza kwamba ushindi wake ni halali

Rais mteule William Ruto kupitia kwa mawakili wake, Fred Ngatia, Katwa Kigen, Kiragu Kimani, Kioko Kilukumi, Melissa Ngania na Kithure Kindiki, ameiambia mahakama hiyo ya majaji saba kuwa alichaguliwa kihalali na iwapo mahakama itakubali maombi ya Odinga na kubatilisha ushindi wake, basi nchi itaingia kwenye mgogoro wa kikatiba kwa kuwa Rais Uhuru Kenyatta bado yuko kwenye ofisi lakini amefungwa mikono kikatiba na hawezi hata kumteua mtu yeyote ofisini.

Na kutokana na mawasilisho ya Odinga kuwa kura ya marudio isifanyike kwa uenyekiti wa Bw Chebukati, Ruto kupitia wakili wake Fred Ngatia, anaeleza kuwa hilo litazua mgogoro mkubwa wa kikatiba.

Katwa Kigen ameieleza mahakama kuwa matokeo ya kura ya urais yaliotangazwa yanatokana uthbitishaji wa fomu 34A zote na hapana chochote kinachoonesha kuwa Ruto alishirikiana na IEBC kuvuna ushindi huo dhidi ya Bw Odinga.

“Walalamishi hawajatoa ushahidi wa kuaminika”

Melissa Ngania, ameieleza mahakama kuwa walalamishi hawajatoa ushahidi wa kuaminika kuifanya mahakama hiyo kubatilisha uchaguzi wa urais.

Kindiki Kithure, ameeleza kuwa makabiliano yaliojitokeza katika ukumbi wa Bomas jijini Nairobi, Agosti 15, ni kama jaribio la mapinduzi kwa sababu maafisa wa ngazi ya juu serikalini wanaripotiwa kukutana na Bw Chebukati, kisiri kwa makusudi ya kumtaka amtangaze Bw Odinga kuwa mshindi wa kura hiyo ama kufanyike kura ya marudio.

Mwishowe, Kioko Kilukumi ameeleza kuwa Odinga na makamishna wanne waliopinga matokeo hayo walijaribu kufanya mapinduzi ya sauti ya raia wa Kenya, lakini Chebukati, Prof Guliye na Molu walisimama kidete hilo kutofanyika.

Aidha, anadai kuwa baraza la kitaifa la ushauri wa usalama liliwateka nyara makamishna wanne wa tume hiyo ili kujaribu kubadilisha matokeo ya kura ya urais.

Vikao hivyo vinakamilika Ijumaa hii.

Imetayarishwa na Kennedy Wandera, VOA, Nairobi

XS
SM
MD
LG