Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumatatu, Desemba 23, 2024 Local time: 05:14

Mawakili wa Ruto: Kesi hii ni ya kupangwa, haina ukweli wowote, sawa na hekaya


Aliyekuwa mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga alipowasilisha mahakamani kesi ya kupinga ushindi wa rais mteule Dr. William Ruto. Aug 22, 2022. PICHA: AP
Aliyekuwa mgombea wa urais nchini Kenya Raila Odinga alipowasilisha mahakamani kesi ya kupinga ushindi wa rais mteule Dr. William Ruto. Aug 22, 2022. PICHA: AP

Mawakili wa rais mteule wa Kenya Dr. William Ruto, wamesema kwamba "kesi iliyo mahakamani kupinga ushindi wa Ruto ni njama iliyopangwa, isiyo na ukweli wowote na sawa na hekaya".

Wakili Fred Ngatia, anayeongoza timu ya mawakili wa Ruto, amesema kwamba kesi ya Raila Odinga kupinga matokeo ya uchaguzi wa urais haina msingi wowote.

Ngatia ameeleza mahakama kwamba kesi hiyo imeundwa kwa kuzingatia tu fikra za watu na wala hakuna Ushahidi wowote.

“Tuonyeshe fomu 34A yoyote ambayo ipo kwenye mfumo wa digitali wa tume ya uchaguzi IEBC na ambayo ni tofauti na fomu iliyotolewa kwenye kituo cha kupigia kura. Ama tuonyeshe sanduku la kupigia kura lililo na kura zinazoonyesha kwamba watu kutoka mahali Fulani au anga Fulani walipiga kura na kwamba udukuzi ulifanyika. Hakuna Ushahidi kama huo. Hii ni kazi ya thamthilia, kazi ya kubuni,” Ngatia ameambia mahakama.

Lengo la Raila ni kuiweka Kenya katika mgogoro wa kikatiba

Wakili huyo ameambia mahakama kwamba kesi ya Raila ina lengo la kuiweka nchi katika mgogoro wa kikatiba.

“Tuna rais ofisini lakini mda wake unamalizika. Hawezi hata kumteua mtu yoyote ofisini.”

“Mlalamishi amesema mara kadhaa kwamba hatashiriki uchaguzi utakaosimamiwa na mwenyekiti wa tume ya uchaguzi IEBC Wafula Chebukati na hataki kukubali kwamba ameshindwa. Anasema kwamba anataka uchaguzi uandaliwe na naibu wa mwenyekiti. Huu utakuwa mgogoro mkubwa wa kikatiba. Mgogoro ambao hatutaki,” amesema Ngatia.

Ngatia anaongoza timu ya mawakili wa Dr. William Ruto ambayo pia inajumulisha mawakili Prof. Kithure Kindiki, Kioko Kilukumi, Katwa Kigen, Kiragu Kimani, Dr Linda Musumba, miongoni mwa wengine.

XS
SM
MD
LG