Katika barua pepe kwa IMF na maafisa wa masuala ya kifedha kutoka kundi la G20 la nchi zilizoendelea kiuchumi, mashirika hayo ya kiraia yamesema nchi maskini tayari zilikuwa nyuma, na sasa masaibu yao yamechangiwa na kupanda kwa bei ya nishati na chakula vinavyochochewa na vita vya Ukraine.
Yamesema kitita cha dola bilioni 650 zilizotolewa mwaka jana na IMF, kiwango cha juu kuwahi kutolewa na taasisi hiyo ya kifedha, zilizisaidia nchi maskini kununua chanjo, kufufua uchumi wao na kuwekeza kwenye mifumo ya afya, lakini msaada zaidi bado unahitajika.
Nchi 99 zenye pato la chini na la kati zilitumia dola bilioni 104 kutoka kwenye akiba yao ya dharura tangu mwezi Agosti, lakini IMF ilitoa dola bilioni 400 kwa nchi zinazoendelea kiuchumi ambazo hazikuwa zinahitaji pesa hizo, mashirika hayo ya kiraia yamesema.