Upatikanaji viungo

Breaking News
Alhamisi, Januari 23, 2025 Local time: 01:07

Mashambulizi yaongezeka Tigray, Ethiopia yakataa juhudi za diplomasia


Ethiopia imesusia juhudi za kidipmolasia kusitisha  vita kaskazini mwa nchi hiyo, na kuendelea kurusha  mabomu katika mji mkuu wa Makelle, eneo la Tigray.

Maelfu ya watu wamekufa, zaidi ya watu 25,000 kukimbilia Sudan kutokeaEthiopia. Kuna ripoti za ukiukwaji wa haki za binadamu tangu waziri mkuu Abiy Ahmed alipoamuru mashambulizi ya anga katika eneo hilo kuanzia Novemba 4 baada ya viongozi wa eneo hilo kudharau mamlaka yake.

Abiy, ambaye ni kiongozi mwenye umri mdogo zaidi Afrika, na alishinda tuzo ya amani ya Nobel mwaka uliopita, amekataa shinikizo la kutaka kufanyika mazungumzo kumaliza vita hivyo ambavyo vinaripotiwa kuenea hadi katika nchi jirani ya Eritrea na kutishia kuyumbisha eneo zima la pembe ya Afrika.

Ethiopia yakataa juhudi za Uganda za mazungumzo

“Tunachosema ni kwamba, mtupe muda. Haitachukua muda mrefu… itakuwa oparesheni ya muda mfupi.” amesema msemaji wa tume maalum ya mgogoro wa Tigray Redwan Hussein akiendelea kusema kwamba “Hatujaiomba Uganda ama nchi yoyote ile kuingilia kati,” baada ya rais wa Uganda Yoweri Museveni kukutana na waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia katika hatua hiyo.

Eritrea imekanusha madai hayo.

Wapiganaji wa Tigray waliripotiwa kufyatua makombora ndani ya Eritrea mwishoni mwa wiki iliyopita.

Umoja wa Afrika, UN watakiwa kuingilia kati

Viongozi wa Tigray wanataka Umoja wa Afrika kuingilia kati na kuishutumu Ethiopia kwa mashambulizi hayo.

Viongozi hao wanasema kwamba wanajeshi wa Ethiopia wanatumia silaha nzito kutekeleza mashambulizi Tigray, ambayo yameharibu bwawa la kuzalisha umeme na kiwanda cha kutengeneza sukari.

Wanamshutumu Abiy, ambaye anatoka kabila kubwa la Oromo, kwa kutekeleza kile wamekitaja kama kuwatesa na kuwaondoa serikalini.

Shirika la Amnesty International limekemea mauaji ambayo pande zote zimelaumiana kutekeleza.

Museveni afuta tweet ya kuitisha mazungumzo

Rais wa Uganda Museveni alikutana na waziri wa mambo ya nje wa Ethiopia Demeke Mekonnen nchini Uganda.

Aliandika kwenye Twitter kwamba “lazima mazungumzo yafanyike na mapigano kukomeshwa ili kuepuka vifo na uharibifu wa uchumi.”

Ujumbe huo umefutwa muda mfupi baadaye. Hakuna sababu imetolewa baada ya tweet ya Museveni kufutwa.

Demeke Aenda Kenya baada ya kutoka Uganda

Kenya na Djibouti zinataka pande husika katika vita vya Ethiopia kusitisha vita na kufanya mazungumzo.

Aliyekuwa rais wa Nigeria Olusegun Obasanjo ameelekea Ethiopia kwa mazungumzo.

“Kila mtu anataka mazungumzo yafanyike. Mazungumzo yanahitajika kwa haraka sana,” amesema Mahboub Maalim, mwanadiplomasia wa Kenya, akiongezea kwamba “sote tunastahili kuwa tunazungumzia kusitisha vita.”

Nchi za ulaya zinaripotiwa kwamba zinapanga kuingilia kati na kujaribu mbinu za kumaliza mzozo huo. Norway imeripoti kwamba inapanga kutuma mjumbe maalum.

Inaripotiwa kwamba jeshi la Ethiopia limedhibithi asilimia 60 ya Tigray na linatarajia kuuteka mji mkuu wa Mekelle baada ya siku tatu za mapigano.

Jeshi la Ethiopia, lenye uzoefu wa kupigana na wapiganaji wa Somalia, na waasi kwenye mpaka na Eritrea, lina karibu wanajeshi 140,000.

Imetayarishwa na Kennes Bwire, VOA, Washington DC

XS
SM
MD
LG