Meya wa Kyiv ametangaza amri ya kutotoka nje kwa saa 35 kuanzia saa mbili usiku majira ya huko.
Milipuko mikubwa ilisikika katikati ya mji wa Kyiv kabla ya alfajiri.
Meya wa Kyiv, Vitali Klitscko amesema “ Leo ni wakati mgumu na mbaya”.
Ameongeza kuwa mji mkuu ambao ni moyo wa Ukraine utalindwa.
Mashahidi wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba waliona jengo la ghorofa likiwaka moto baada ya kushambuliwa kwa mizinga.
Zima moto walijaribu kuzima moto huo na wafanyakazi wa ukoaji walisaidia kuwaondoa wakazi waliokwama ndani kwa kutumia ngazi.
Kyiv iliepushwa na mapigano mabaya tangu Rashia kuivamia Ukraine hapo Februari 24, lakini jeshi la Rashia linaukaribia polepole mji huo na mashambulizi ya makombora yameongezeka.
Maelfu ya watu wameuawa katika mgogoro huo na mamilioni wengine walikimbia.