Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Desemba 21, 2024 Local time: 19:09

Mashabiki wailaumu Bafana Bafana kushindwa kutumia nafasi vizuri


Mwamuzi wa Misri akimwonyesha kadi nyekundu beki wa Afrika Kusini Grant Kekana (kushoto) wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) 2024 Februari 7,2024. Picha na Issouf SANOGO / AFP
Mwamuzi wa Misri akimwonyesha kadi nyekundu beki wa Afrika Kusini Grant Kekana (kushoto) wakati wa mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Mataifa ya Afrika (CAN) 2024 Februari 7,2024. Picha na Issouf SANOGO / AFP

Baada ya timu ya taifa ya Afrika Kusini Bafana Bafana kushindwa kufuzu kwenda fainali Jumatano huko Ivory Coast, raia wa Afrika Kusini wamepeleka lawama zao kwa wachezaji kwa kile wanachodai, hawakutumia nafasi walizopata kuweka mpira kimyani huku wengine wakisema Afrika Kusini ilikosa bahati.

Bafana Bafana iliondolewa kwa penati nne kwa mbili, zilizofungwa na wachezaji wa timu ya taifa ya Nigeria Super Eagles katika mchezo wa awali wa nusu fainali.

Ni mchezo uliosisimua wengi kabla, wakati, na baada ya kumalizika kwake, kwani tambo za mashabiki wa pande mbili zilikuwa nyingi mitandaoni, hatua iliyopelekea ubalozi wa Nigeria Pretoria kutoa tangazo ukiwataka Wanaijeria waishio humu nchini kuwa makini.

Baada ya kumalizika kwa mbungi hilo Afrika Kusini ikiwa imeshindwa kufuzu kwenda fainali kufuatia kipigo cha penati 4 kwa 2 walichopokea kutoka kwa Super Eagles ya Nigeria baada ya dakika 120 kumalizika wakiwa wametoshana nguvu ya kufungana goli moja moja.

Liston Mabaso ni mmoja wa washabiki wa Bafana Bafana wamesema Afrika Kusini haikutumia vizuri nafasi ilizopata.

Lakini hata hivyo sio wote wanaowalalamikia wachezaji wa Bafana Bafana, Vincent Ndebere mkazi wa Pretoria anasema katika mchezo wa jana Afrika Kusini ilicheza vizuri.

“Hatumlaumu yeyote, mchezo ulikuwa sawa kwa pande zote, ila hatukushinda penati na mchezo ulikuwa mzuri,” alisema Ndebere

Japo haikupigiwa upatu wa kupata ushindi dhidi ya Nigeria, mchambuzi wa soka na mwandishi habari mkongwe wa shirika la utangazaji la Afrika Kusini SABC, Fortunatus Kansonfi anasema Afrika Kusini ilionesha kiwango cha juu sana.

“Kitakwimu bafana bafana waliingia uwanjani ikiwa haipewi nafasi ya kushinda dhidi ya Nigeria lakini mwenendo waliokwenda nao baada ya kuitoa Morocco ilileta taswira kwamba Bafana anaweza akapeleka tena kilio kwa mabingwa wengine” alisema Kansonfi

Pamoja na kipute cha jana, timu hizo zimekutana mara 15, Nigeria ikiwacharaza Afrika Kusini mara 8, huku ikipoteza michezo miwili na zimeshatoka suluhu mara tano.

Kwa mujibu wa wachambuzi wa kandanda hapa Afrika Kusini, muda ni sasa kwa Bafana Bafana, kutafuta washambuliaji wenye uwezo wa kufunga magoli.

Aliongeza Kansonfi kwa kusema kuwa “Sehemu ambayo Afrika Kusini inapaswa kurekebisha ni ya ushambuliaji, mshambuliaji aliyekuwepo jana hakuwa na mikiki mikiki ya kupenya katika ngome ya Nigeria, nafasi walizopata laity zingemkuta mshambuliaji wa hali ya juu, yawezekana Bafana bafana wangeibuka kidedea mpaka dakika 90 za mwanzo”.

Wakati huo huo jeshi la uhamiaji, polisi wa jiji na wale wa kawaida, leo wamemwagwa katika maeneo mbali mbali ya jiji la Pretoria, wakikamata wageni wasio na vibali halali vya kuishi hapa Afrika Kusini hatua ambayo wageni kutoka nchi za kiafrika wamesema kinahusiana na kitendo cha Afrika Kusini kufungwa na Nigeria katika mchezo wa nusu fainali jana kama ilivyotabiriwa siku chache zilizopita kuwa huenda hilo likatokea.

Forum

XS
SM
MD
LG