Ni wiki ambayo aliyekuwa makamu wa rais wa Uganda Gilbert Balisekka Bukenya angependa kuisahau maishani mwake. Shida zaonekana kumwandama Prof Bukenya kutoka pande zote.
Siku ya Jumatatu mahakama ya kupambana na ufisadi ilitupilia mbali dhamana iliyompa Bukenya mwezi wa sita alipofika mbele ya mahakama hii kujibu mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi. Siku ya jumatano, mahakama kuu nayo ikasema Bukenya aliwaonga wapiga kura kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi wa pili kwa hivyo hakuwa na haki ya kuendelea kuwa mbunge wa eneo la Busiro ya kaskazini.
Mwezi wa tano ni mwezi ulio muhimu sana maishani mwa Bukenya. Alizaliwa mwezi wa tano, akachaguliwa kuwa makamu wa rais mwezi wa tano mwaka wa elfu mbili na tatu na kufutwa kazi mwezi wa tano mwaka huu. Mwezi huo huo, mahakama ya kupambana na ufisadi ilimuamrisha kufika kwenye mahakama hiyo kujibu mashtaka ya matumizi mabaya ya ofisi.
Prof Gilbert Bukenya mwenye umri wa miaka sitini na miwili kando na kuwa mwanasiasa, ni daktari lakini daktari huyu anakumbana na ugonjwa ambao hawezi kujitibu- Ugonjwa wa matumizi mabaya wa ofisi ingawa kunao watu wanaosema ni fitina za kisiasa.
Inasemekana Bukenya alikiuka utaratibu maalum unaotumiwa na serikali wakati inapotoa kandarasi na kutumia ofisi yake kuathiri uamuzi wa ni kampuni gani ingepata kandarasi ya kutoa magari na piki piki zilizotumiwa na marais wa nchi zilizo wanachama wa jumuiya ya madola wakati walipofanya mkutano wao nchini Uganda mwezi wa kumi na moja mwaka wa elfu mbili na saba.
Alipofikishwa mahakamani siku ya kwanza Bukenya alipewa dhamana. Kisha alikwenda kwenye mahakama ya kikatiba kuomba mashtaka dhidi yake yatupiliwe mbali akisema kama mwenyekiti wa kamati ya kuandaa mkutano wa jumuiya ya madola, alishikilia wadhifa huo kwa niaba ya rais Yoweri Museveni na kulingana na sheria alikuwa na kinga.
Kwenye uamuzi wake, mahakama ya kikatiba ikaamua kuwa makamu wa rais hana kinga kulingana na sheria na matokeo yake; Bukenya akarudishwa kwenye mahakama ya kupambana na ufisadi. Siku ya jumatatu wiki hii, alipofika mbele ya hakimu Irene Akankwasa kwenye mahakama ya kupambana na ufisadi hakimu akaamua mashtaka anayokumbana nayo yanafaa kusikilizwa kwenye mahakama kuu kwa hivyo dhamana aliyopewa na mahakama ya kupambana na ufisadi ambayo ni mahakama ya chini haingetumiwa na mahakama kuu.
Alimshauri Bukenya kuomba dhamana kutoka mahakama kuu kwa sababu kesi yake sasa yafaa kusikilizwa huko. Uamuzi huu ndio uliompeleka rumande Prof Bukenya. Maoni ya wabunge kuhusu kuzuiwa kwa Bukenya “Kufungwa kwa aliyekuwa makamu wa rais Gilbert Bukenya ikiwa ni kulingana na sheria basi wacha sheria ifuatwe. Lakini swali letu ni je...wako wapi wale wengine walioshtakiwa na Bukenya? Kwa nini kumshtaki Bukenya peke yake ilhali tunajua kesi hii inawahusisha watu wengine.”
Hapo jana ofisi ya mkaguzi mkuu wa serikali ikawafungulia mashtaka mawaziri watatu mkiwemo waziri wa mambo ya nje Sam Kuteesa, mratibu mkuu wa chama tawala bungeni John Nasasira na waziri wa Leba Mwesigwa Rukutana. Habari za kushtakiwa kwa watu wengine huenda zilimliwaza Bukenya kwa muda lakini kabla ya jua kutua hapo jana... mahakama kuu ikaamua kuwa Prof. Gilbert Bukenya hakuwa na haki ya kuendelea kuwa mbunge wa eneo la bunge la Busiro ya kaskazini kwa sababu mpinzani wake kwenye uchaguzi mkuu wa mwezi wa pili.
Caster Hussein Bukenya alitoa ushahidi wa kutosha kuwa Prof Bukenya aliwahonga wapiga kura jambo lililoathiri matokeo ya uchaguzi.Wakili wa Prof. Bukenya anajaribu kuona ikiwa Bukenya atapata dhamana kwa sababu anaugua ugonjwa wa shinikizo la damu. Haijulikani ni lini atakapoipata dhamana lakini kwa sasa Bukenya ametulia gerezani Luzira baada ya kuushikilia wadhifa wa makamu wa rais kwa miaka minane.