Upatikanaji viungo

Breaking News
Jumamosi, Novemba 23, 2024 Local time: 19:48

Marekani yawekea Eritrea vikwazo kutokana na mzozo wa Tigray


Mwanajeshi wa Eritrea akiwa mbele ya majengo yaliyo haribiwa na mapigano
Mwanajeshi wa Eritrea akiwa mbele ya majengo yaliyo haribiwa na mapigano

Marekani Jumatatu imeweka vikwazo vipya kwa Eritrea kutokana na ghasia za Tigray kaskazini mwa Ethiopia.

Hatua imechukuliwa wakati maelfu ya watu kwenye eneo hilo wakikabiliwa na njaa kutokana na kuzuiliwa kwa upelekaji wa misaada na serikali, huku mapigano yakiendelea kuenea kwenye maeneo mengine nchini humo.

Kwa mujibu wa shirika la habari la AP,taarifa kutoka kwa wizara ya fedha ya Marekani imesema kuwa mkuu wa jeshi la Eritrea, Filipos Woldeyohannes amewekewa vikwazo chini ya sheria ya kimataifa ya haki za binadamu, kwa kuongoza kikosi kilicho tekeleza ukatili usioelezeka, ukiwemo mauaji, dhuluma za kingono pamoja na kuuwawa kwa wavulana.

Taarifa hiyo pia imeomba Eritrea kuondoa wanajeshi wake kutoka eneo la Tigray, Ethiopia. Mapigano ya Tigray yameua maelfu ya watu na kuacha waangalizi wakiwa wameshangaa kutokana na kuwa waziri mkuu wa Ethiopia Abiy Ahmed, ambaye ni mshindi wa tuzo ya Nobel, ameshirikiana na Eritrea ambayo ni hasimu wa zamani wa Ethiopia, kupigana na vikosi vya Tigray ambapo pia raiya wa kawaida wameathirika.

Baadhi ya mashuhuda wameliambia shirika la habari la Reuters kwamba kumekuwa na ukatili kama vile ubakaji , uharibifu wa vituo vya afya, uharibifu wa mimea mashambani pamoja na watu kufukuzwa makwao.

Hata hivyo serikali ya Ethiopia imekuwa ikikanusha kuwepo kwa vikosi vyake huko Tigray kwa miezi kadhaa. Eritrea kwa upande wake kupitia wizara ya mambo ya kigeni pia imekanusha madai hayo, wakati ikiambia Marekani itoe ushahidi wa kutosha.

Mapema mwaka huu Marekani iliashiria kupoteza subira kwa Ethiopia wakati ikisitisha msaada wa mamilioni ya dola za kiusalama pamoja na kuwekea vikwazo kwa baadhi ya maafisa wa ngazi za juu ambao hawakutajwa.

XS
SM
MD
LG